'Iyd Taratibu Na Shari'ah Zake
Imetafsiriwa na: Ummu Ummu Ayman
Sifa njema ni za Allaah, Bwana wa Ulimwengu, na rehma na amani zimshukie Mtume wetu Muhammad na Aali zake na Swahaba zake.
“'Iyd” ni neno la kiarabu linalomaanisha jambo la kitabia au ada, lenye kurudi na kujirejea. 'Iyd au sikukuu ni alama au nembo inayopatikana katika kila taifa, ikiwa ni pamoja na mataifa yale yaliyotajwa katika vitabu vitukufu na yale ya waabudiao masanamu, pamoja na wengineo, kwa sababu kusherehekea sikukuu ni jambo la kimaumbile katika maumbile ya mwanaadamu. Watu wote wanapenda kuwa na matukio maalumu ya kufanya sherehe, ambapo wanaweza kukukusanyika pamoja na kuonyesha furaha zao.
Sikukuu za mataifa ya makafiri zinaweza kufungamanishwa na mambo ya kidunia, kama kuanza kwa mwaka, kuanza kwa msimu wa kilimo, kubadilika kwa hali ya hewa, kuanzishwa kwa dola, kutawazwa kwa kiongozi, n.k. Zinaweza pia kufungamanishwa na matukio ya kidini, kama ambavyo nyingi ya sikukuu zinazowahusu Mayahudi na Wakiristo tu, mfano Alkhamiys ambayo wanadai kuwa meza maalum iliteremshwa kwa Yesu, Krismas, Mwaka Mpya, Siku ya kushukuriana, na sikukuu ambazo watu hupeana zawadi. Hizi husherehekewa katika nchi zote za Ulaya na Amerika ya Kaskazini hivi sasa, na katika nchi nyengine ambazo ukristo una nguvu, hata kama nchi yenyewe si ya kikiristo kiuhalisi. Baadhi ya wanaoitwa Waislam huweza kujiunga katika sikukuu hizi, kwa sababu ya ujinga au unafiki.
Wamagiani (Magians) nao pia wana sikukuu zao, kama Mahrajaan, Namrud n.k.
Ma-baatini (Miongoni mwa Mashia) wana sikukuu zao pia, kama ‘Iyd al-Ghadiyr, ambapo wanadai kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amempa ukhalifa ‘Ali (Radhiya Allaahu ‘anhu) na maimamu kumi na moja baada yake.
Waislamu Wanatambulika Kwa Sikukuu Zao
Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) "Kila Umma una sikukuu yake na hii ni sikukuu yenu" yanaonyesha kuwa ‘Iyd hizi mbili ni maalumu kwa Waislamu tu, na kuwa hairuhusiwi kwa Muislam kuwaiga makafiri na washirikina katika jambo lolote ambalo ni maalumu ndani ya sherehe zao, iwapo kama ni chakula, nguo, kuwasha moto au matendo ya ibada.
Watoto wa Kiislam wasiruhusiwe kucheza katika sikukuu hizo za kikafiri, au kujipamba, au kujumuika na makafiri katika matukio hayo. Sikukuu zote za kikafiri au zilizozushwa ni haraam, mfano kama sherehe za Siku ya Uhuru, maadhimisho ya mapinduzi, miti ya sherehe za sikukuu au kutawazwa kwa kiongozi, siku za kuzaliwa, Sikukuu ya Wafanyakazi, Sikukuu ya Nile, Shamm an-Nasiym (sikukuu ya majira ya baridi ya Wamisri), siku ya walimu, na Maulidi ya Mtume (Kuzaliwa kwa Mtume).
Waislam hawana sikukuu ukiacha ile ya ‘Iyd al-Fitwr na ‘Iyd al-Adhw-haa, kwa sababu ya hadiyth iliyotolewa na Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: "Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja Madiynah na watu walikuwa na siku mbili wakicheza na kufurahi. Akauliza, "Ni siku gani hizi mbili?" Wakasema, "Tulikuwa tukicheza na kufurahi katika siku hizi zama za ujaahiliyya" (zama za ujinga kabla ya Uislamu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, "Allaah Amekupeni siku bora kuliko hizo, nazo ni siku ya ‘Iyd Al-Adhw-haa na siku ya ‘Iyd Al Fitwr". (Sunan Abi Daawuud 1134)
Yafuatayo ni maelezo kuhusu shari'ah na adabu za ‘Iyd mbili kwa mujibu wa Sharia ya Kiislam:
Ahkaamul-'Iyd (Shari'ah Katika 'Iyd)
Kufunga
Ni haraam kufunga katika siku za ‘Iyd kutokana na hadiyth ya Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu), amesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kufunga katika siku ya Fitwr na katika siku ya Kuchinja (Adhw-haa). (Imeripotiwa na Muslim, 827)
Shari'ah Katika Swalah Za 'Iyd
Baadhi ya wanavyuoni wanasema kuwa Swalah ya ‘Iyd ni waajib, huu ni mtizamo wa wanavyuoni wa Kihanafi na Shaykh al-Islam Ibn Taymiyah (rahimahu Allaah). Wanasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalah zote za ‘Iyd na hakuacha kufanya hivyo hata mara moja. Wamechukua ushahidi katika ayah (yenye tafsiri),
"Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi" Al-Kawthar: 2
Yaani Swalah ya ‘Iyd na kuchinja baada yake, ambayo ni amri, na kwa ukweli kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamrisha wanawake watolewe kuhudhuria Swalah ya ‘Iyd, na kwamba mwanamke aliyekuwa hana jilbaab aazime kutoka kwa ndugu yake
Baadhi ya wanavyuoni wanasema kuwa Swalah ya ‘Iyd ni Fardhu Kifaayah (fardhi yenye kutosheleza). Huu ni mtizamo wa Kihanbali. Kundi la tatu linasema kuwa Swalah ya ‘Iyd ni Sunnah iliyokokotezwa. Huu ni mtizamo wa Kimaalik na Kishaafi. Wanachukua ushahidi ya hadiyth ya Bedui inayosema kuwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Hakufaradhisha Swalah yoyote kwa waja Wake zaidi ya zile Swalah tano. Kwa hiyo Waislam wafanye hima kuhudhuria Swalah ya ‘Iyd, hususan kwa kuwa maoni ya kuwa ni waajib yameegemea katika ushahidi wenye nguvu. Neema, baraka na malipo makubwa yanapatikana kwa kuhudhuria Swalah za ‘Iyd, na kwa ukweli kuwa mtu atakuwa anafuata mwendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufanya hivyo, basi inatosha kuwa ni changamoto.
Mambo Ya Lazima Na Wakati Wa Swalah Ya 'Iyd
Baadhi ya wanavyuoni wa Kihanbali wanasema kuwa sharti za Swalah ya ‘Iyd ni iqaamah lazima isomwe na ni lazima iswaliwe kwa jamaa. Baadhi yao wamesema kuwa sharti za Swalah ya ‘Iyd ni sawa na zile za Swalah ya Ijumaa, isipokuwa katika khutba, ambapo kuihudhuria si lazima. Wengi miongoni mwa wanavyuoni wanasema wakati wa Swalah ya ‘Iyd unaanza pale jua linapochomoza kwa masafa ya urefu wa mshale, kwa linavyoonekana kwa macho matupu, na unaendelea mpaka jua linapokaribia kuwa sawa sawa.
Maelezo Ya Swalah Ya 'Iyd
‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “ Swalah ya ‘Iyd Fitwr na al-Adhw-haa ni rakaa mbili zilizotimia, sio fupi fupi. Hii ni kwa mujibu wa maneno ya Mtume, na muongo ni mwenye kulaaniwa.”
Abu Sa’iyd amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekuwa akija katika pahala pa kuswalia katika siku za Fitwr na al-Adhw-haa, na jambo la mwanzo analofanya ni kuswali”.
Takbira inarejewa mara saba katika rakaa ya mwanzo na mara tano katika rakaa ya pili, Qur-aan inasomwa baada yake katika kila rakaa.
Imeripotiwa kutoka kwa A’ishah: Takbira ya al-Fitwr na al-Adhw-haa ni mara saba katika rakaa ya mwanzo na mara tano katika rakaa ya pili, mbali na Takbira ya rukuu. (imeripotiwa na Abu Daawuud; imesahihishwa na jumla ya isnaad)
Iwapo mtu amejiunga na Swalah amemuwahi Imaam wakati wa Takbira hizi za ziada, ni juu yake kusema “Allaahu Akbar” pamoja na Imaam, na halazimiki kuzilipa Takbira ambazo zimempita, kwa sababu (takbira hizo) ni Sunnah, sio waajib. Kuhusu nini kinatakiwa kisemwe baina ya Takbira, Hammaad ibn Salamah ameripoti kutoka kwa Ibraahiym kuwa "Waliyd ibn ‘Uqbah aliingia msikitini wakati Ibn Mas’uud, Hudhayfah na Abu Muusa wapo hapo, na akasema, “‘Iyd ipo hapa, nini natakiwa kufanya?” Ibn Mas’uud akasema: “Sema ‘Allaahu Akbar’, msifu na mshukuru Allaah, msalie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na omba du’aa, kisha sema ‘Allaahu Akbar’, msifu na mshukuru Allaah, mswalie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)….n.k.’ (Imeripotiwa na at-Twabaraaniy. Ni hadiyth sahihi iliyonukuliwa katika al-Irwaa’ na kwengineko).
Kusoma Qur-aan Katika Swalah Za 'Iyd
Imependekezwa (mustahabb) kuwa katika Swalah za ‘Iyd, imaam asome surat Qaaf (sura ya 50) na surat al-Qamar (sura ya 54), kama ilivyoripotiwa katika Swahiyh Muslim kuwa ‘Umar ibn Al-Khattwaab alimuuliza Abu Waaqid al-Laythi, “Nini Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika [‘Iyd] al-Adhw-haa na al-Fitwr?” Akasema, “Alikuwa akisoma Qaaf, Wal-Qur-aan al-Majiyd [Qaaf 50:1] na Iqtarabat as-saa’ah wa’nshaqq al-qamar [al-Qamar 54:1].
Ripoti nyingi zinaonyesha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma Surat al A’laa [87] na Suurat al-Ghaashiyah {88], kama ambavyo alivyokuwa akizisoma katika Swalah ya Ijumaa. An-Nu’maan ibn Bashiyr amesema:
"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika '‘Iyd mbili na siku ya Ijumaa Sabbih Isma Rabbikal-a'laa (Al-A'alaa 87:1) na Hal Ataaka Hadiythul-Ghaashiyah (Al-Ghaashiyah 88:1)" Swahiyh Muslim 878
Samurah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika ‘Iyd mbili Sabbih Isma Rabbikal-a'alaa (Al-a'alaa 87:1) na Hal Ataaka Hadiythul-Ghaashiyah (Al-Ghaashiyah 88:1) Imesimuliwa na Ahmad na wengine ni Swahiyh [ Al-Irwaa 3/116]
Swalah Inaswaliwa Kabla Ya Khutbah
Moja ya shari'ah za ‘Iyd ni kuwa Swalah ni lazima iwe kabla ya khutbah, kama ilivyoripotiwa katika Musnad Ahmad kutoka katika hadiyth ya Ibn ‘Abbaas, ambaye ameshuhudia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali kabla ya khutba siku ya ‘Iyd kisha akatoa khutba (Musnad Ahmad 1905. Hadiyth hii pia iko katika Swahiyh mbili)
Yeyote Anayetaka Kuondoka Wakati Wa Khutbah Ameruhusiwa Kufanya Hivyo
‘Abd-Allaah ibn al-Saab amesema: "Nilihudhuria '‘Iyd pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alipomaliza alisema, tutatoa khutba, kwa hiyo anayetaka kukaa (na kusikiliza) khutba basi akae na anayetaka kuondoka basi aondoke (Irwaa al Ghaliyl 3/96)
Swalah Isicheleweshwe Kwa Muda Mrefu
‘Abd-Allaah ibn Bishr, swahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alitoka pamoja na watu siku ya al-Fitwr au al-Adhw-haa, na akaonyesha kutopendezwa kwa kuwa Imaam alikuja akiwa amechelewa sana. Akasema: "Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tungelikuwa tumeshamaliza wakati wa sasa" na huo ulikuwa wakati wa Tasbiyh” (Imesimuliwa na na Al-Bukhaariy).
Swalah Za Sunnah, Pahala Pa Swalah (Ya 'Iyd)
Hakuna Swalah za Sunnah ambazo zinaswaliwa kabla au baada ya Swalah ya ‘Iyd, kama alivyoripoti Ibn ‘Abbaas kuwa "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitoka katika siku ya ‘Iyd na akaswali rakaa mbili, bila ya chochote (Swalah yoyote) kabla au baada yake". Hali hii ni iwapo Swalah itaswaliwa pahala pa kuswaliwa au sehemu ya wazi. Hata hivyo, iwapo watu wataswali ‘Iyd msikitini, basi watatakiwa waswali rakaa mbili za Tahiyat al-Masjid (Swalah ya kiamkizi cha msikiti) kabla hawajakaa kitako.
Iwapo Watu Hawatokuwa Na Habari Ya 'Iyd Mpaka Siku Ya Pili
Abu ‘Umayr ibn Anas ameripoti kutoka kwa ‘ami yake miongoni mwa Answaar kuwa alisema: "Kulikuwa na mawingu na hatukuweza kuuona mwezi wa Shawwaal, kwa hiyo tukaanza siku kwa kufunga, kisha ukaja msafara mwisho wa siku na wakamwabia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa wameona mwezi wa Shawwaal siku moja kabla, akawaambia watu waache kufunga na wakaenda kuswali ‘Iyd siku ya pili" Imeripotiwa na Maimaam watano, ni Sahiyh; Al-Irwaa' 3/102
Iwapo mtu amekosa Swalah ya ‘Iyd, mtazamo ulio sahihi kuliko yote ni kuwa anaweza kuilipa kwa kuswali rakaa mbili.
Kuhudhuria Kwa Wanawake Katika Swalah Za 'Iyd
Hafswah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema: "Tulikuwa tukiwazuia wasichana wenye hedhi kuhudhuria Swalah za ‘Iyd. Kisha akaja mwanamke kukaa katika ngome ya Banu Khalaf na akatuambia kuhusu dada yake. Mume wa dada yake alihudhuria vita kumi na mbili pamoja na Mtume (na akasema) , Dada yangu alikuwa naye katika vita sita. Akasema tulikuwa tukiwatendea walioumia na tukiwashughulikia wagonjwa. Dada yangu alimuuliza Mtume kama kuna ubaya wowote kutokwenda kuswali ‘Iyd ikiwa hana jilbaab. Akasema "mwache rafiki yake ampe moja wa jilbaab lake ili aweze kushuhudia baraka za ‘Iyd na aone kujumuika kwa Waislamu" Ummu 'Atwiyah alipokuja nilimuuliza umemiskia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema hivyo?" Akasema "Baba yangu achinjwe kwa ajili yake" Na alikuwa hamtaji ila baada ya kusema "baba yangu achinjwe kwa ajili yake". "Nimemsikia akisema kuwa wasichana na wale wanaotawishwa au wasichana waliotawishwa na wanawake wenye hedhi ili washuhudie baraka za ‘Iyd na kujumuika kwa waumini. Lakini wale wenye hedhi wakae mbali na sehemu ya kuswali" (Swahiyh Al-Bukhaariy)
Vijana wa kike (‘awaatik, mmoja ‘aatiq) ni wale waliokwisha vunja ungo au wako karibu na kufanya hivyo, au wamefikia umri wa kuolewa, au walio na thamani katika familia zao, au wasiofanyishwa kazi zisizo na heshima. Inaonekana kuwa wamekuwa wakizuiwa vijana hawa kutoka nje kwa sababu ya uovu uliojitokeza baada ya kizazi cha kwanza cha Uislam; lakini Swahaabah hawakukubaliana na hilo na wakaona kuwa shari'ah ya wakati wao lazima ibaki kama ilivyokuwa wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
“Jilbaab lake”- ametakiwa kuazima baadhi ya nguo ambazo hakuwa akizihitajia.
“Wanaotengwa/Wanaotawishwa”- ambao wanaowekewa paazia kipembeni mwa nyumba ambamo wari hukaa nyuma yake.
“Wanawake walio katika hedhi”- huyyadh, mmoja haaidh– hii inaweza kurejea kwa vijana wa kike waliofikia umri wa kukua, au wanawake waliomo katika siku zao na wasio tohara.
“Wanawake walio katika hedhi wanatakiwa wajitenge na Swalah – pahala penyewe” – Ibn al-Munayyir amesema: "Sababu ya kujitenga na sehemu ya kuswali ni kuwa wakisimama pamoja na wanawake wanaoswali japokuwa hawaswali, itaonekana kuwa hawana heshima na Swalah au hawajali kwa hiyo ni bora kwao kuepuka kufanya hivyo"
Imesemekana kuwa sababu ya kutakiwa wanawake walio katika hedhi kujitenga na sehemu ya kuswalia ni tahadhari, kuwa wanawake wasije karibu ya wanaume bila ya sababu iwapo wao hawaswali, au wasiwaudhi wengine kwa damu au harufu yake.
Hadiyth hii inamtaka kila mmoja kuhudhuria Swalah ya ‘Iyd, na kushirikiana baina yao katika wema na ucha Mungu. Wanawake walio katika hedhi wasiachwe nyuma katika kumtaja Allaah au sehemu njema kama mikusanyiko yenye madhumuni ya kutafuta elimu na kumtaja Allaah – ukiachia misikitini. Hadiyth hii pia inaonyesha kuwa wanawake wasitoke nje bila ya jilbaab.
Hadiyth hii inatuambia kuwa sio sawa kwa vijana wa kike na wanawake wanaotawishwa kutoka nje bila ya sababu inayokubalika. Inasema kuwa imependekezwa (mustahabb) kwa wanawake kuvaa jilbaab, na kuwa imeruhusiwa kuazimana nguo. Pia imeonyesha kuwa Swalah ya ‘Iyd ni wajibu.
Ibn Abi Shaybah pia ameeleza kuwa Ibn ‘Umar alikuwa akienda na yeyote anayeweza kwenda naye katika wanawake wa nyumbani kwake katika Swalah za ‘Iyd.
Hadiyth ya Umm ‘Atwiyah pia inaeleza sababu ya shari'ah hii, ni kuwa ili wanawake waweze kushuhudia baraka ya ‘Iyd, waone mkusanyiko wa Waislam, na wapate nao baraka na utukufu wa siku hii.
At-Tirmidhiy (Mwenyeezi Mungu Amrehemu) alisema katina Sunan yake, baada ya kutaja Hadiyth ya Umm 'Atwiyah, "baadhi ya 'Ulamaa wamechukulia Hadiyth hii na kuwaruhusu wanawake waende katika Swalah za ‘Iyd na wengineo hawakupendezewa. Imeripotiwa kuwa 'Abdullah Ibn Al Mubaarak alisema, 'Sipendi wanawake waende katika Swalah za ‘Iyd siku hizi. Na mwanamke akishikilia kwenda basi mumewe amwachilie kwenda lakini anapokwenda avae nguo zake kukuuu kabisa na asijipambe. Na akishikilia kujipamba basi asitoke nje. Na hali hii mume anayo haki kumzuia kutoka nje. Imeripotiwa kuwa bibi 'Aishah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, "Kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeliona hali za wanawake walivyo hivi sasa angeliwazuia kwenda misikitini kama vile wanawake wa Bani Israaiyl walivyozuiliwa" Imeripotiwa kwamba Sufyaan Ath-Thawriy hakupendezewa wanawake kwenda kuswali Swalah za ‘Iyd. (At-Tirmidhiy 495)
Umm ‘Atwiyah ametoa fatwa yake katika hadiyth iliyotajwa hapo juu, muda baada ya kufa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki, na haikuripotiwa kuwa yeyote miongoni mwa Maswahaba amepingana na fatwa hii. Maneno ya ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha), “Iwapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeona yanayofanyika kwa wanawake, angewazuilia kwenda misikitini”, hayapingi hii fatwa (alimradi tu wanawake wanatimiza masharti ya Kiislamu ya kutoka kwao nje) Ni vizuri zaidi iwapo ruhusa itatolewa kwa wale wanawake wasiotoka kwa ajili ya kuwaangalia wanaume au kuangaliwa wao, ambao kuhudhuria kwao hakutopelekea uovu wowote na wasiokwenda kusongamana na wanaume mitaani au msikitini (yaani wanawake ambao kutoka kwao hakutosababisha fitna au kishawishi kwake au kwa wanaume).
Wanaume wawakague wanawake wao wanapotoka nje kwa ajili ya Swalah kuhakikisha kuwa hijabu zao ziko kamili, kwa sababu wao ndio “wachungaji” wenye jukumu kwa “machunga” wao. Wanawake wanatakiwa watoke wakiwa katika nguo zisizovutia, wasiwe wamejipamba au kujitia manukato. Wanawake walio katika hedhi wasiingie msikitini au sehemu ya kuswalia; wanaweza kungojea ndani ya gari, kwa mfano, ambapo wanaweza kusikia khutbah.
ADAAB ZA 'IYD
Kukoga
Moja ya heshima za ‘Iyd ni kukoga kabla ya kwenda katika Swalah. Imeripotiwa katika ripoti sahihi katika al-Muwatta’ na kwengineko kuwa ‘Abd-Allaah ibn ‘Umar alikuwa akikoga siku ya al-Fitwr kabla ya kuja pahala pa kuswalia. (al-Muwattwa’428)
Imeripotiwa kuwa Sa'iyd ibn Jubayr alisema "Mambo matatu ni Sunnah siku ya ‘Iyd; kwenda kwa miguu katika uwanja wa kuswali (MuSwallaa), kukoga, na kula kabla ya kutoka nje". Hivi ndivyo alivyosema Sa'iyd ibn Jubayr na labda amejifunza haya kutoka kwa baadhi ya Maswahaba.
An-Nawawiy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ametaja kuwa wanavyuoni wamekubaliana kuwa imependekezwa (mustahab) kukoga kabla ya Swalah ya ‘Iyd.
Sababu ya kuwa ni mustahab kukoga kabla ya Swalah ya Ijumaa na mikusanyiko mengine pia inahusika katika suala la ‘Iyd vilevile.
Kula Kabla Ya Kutoka
Mtu asitoke kwenda pahala pa kuswalia ‘Iyd al-Fitwr kabla ya kula tende, kwa sababu ya hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy kutoka kwa Anas ibn Maalik ambaye amesema:
"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hatoki asubuhi ya ‘Iyd Al Fitwr mpaka ale tende na alikuwa kila kwa hesabu ya witri. (Al-Bukhaariy, 953)
Imependekezwa (mustahab) kula kabla ya kutoka kwa sababu hii inahakikisha kuwa hatukuruhusiwa kufunga katika siku hiyo, na ni onyesho kuwa Swawm sasa imemalizika. Ibn Hajar (rahimahu Allaah) ameeleza kuwa hii ni kwa ajili ya kuwakinga watu kuendeleza Swawm na pia inamaanisha utii kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). (Fat-hul-Baariy, 2/446).
Iwapo mtu hatakuwa na tende, anaweza kufutari kwa chochote kilichoruhusiwa. Kwa upande mwengine, katika ‘Iyd al-Adhw-haa, imependekezwa mtu asile mpaka baada ya Swalah, ambapo mtu anatakiwa kula nyama ya mnyama mmojawapo aliyechinjwa (kwa ajili ya siku hii).
Takbira (Allaahu Akbar) Katika Siku Ya 'Iyd
Hii ni moja ya Sunnah kubwa kabisa ya siku hii, kwa sababu ya maneno ya Allaah (yenye tafsiri):
"......Mwenyezi Mungu Anakutakieni yaliyo mepesi wala Hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate kushukuru" [Al-Baqarah 2:185].
Ad-Daaraqutniy na wengine wameripoti kuwa wakati Ibn ‘Umar alipokuwa akitoka katika ‘Iyd al-Fitwr na al-Adhw-haa, huwa anajitahidi kutoa Takbiyr mpaka anapofika pahala pa kuswalia, kisha kuendelea na Takbiyr mpaka aje Imaam.
Tendo la kupiga Takbira kutoka nyumbani hadi pahala pa kuswalia, na mpaka Imaam aingie, ni maarufu miongoni mwa Salaf (waliotangulia wema) na limeripotiwa na waandishi wengi kama Ibn Abi Shaybah, ‘Abdur-Razzaaq na al-Firyaabi katika kitabu chake Ahkaam al-‘‘Iydayn kutoka katika kundi la Salaf. Moja ya mfano wake ni ripoti kuwa Naafi’ ibn Jubayr alikuwa akitoa Takbira na alikuwa akishangaa kwa nini watu hawafanyi hivyo. Alikuwa akiwaambia watu, "Kwa nini hamfanyi Takbira? Ibn Shihaab Az-Zuhri kasema, "Watu walikuwa wakipiga takbira kuanzia wakati wanapotoka majumbani mwao hadi anapoingia Imaam".
Wakati wa kutoa Takbira katika ‘Iyd al-Fitwr unaanza usiku wa kuamkia ‘Iyd mpaka wakati Imaam anapofika kuongoza Swalah.
Maneno Ya Takbira
Ibn Abi Shaybah ameripoti katika al-Muswannaf kuwa Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akitamka takbira katika siku za Tashriiq kama ifuatavyo: “Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, laa ilaaha illa-Allaah, wa Allaahu Akbar, Allaahu Akbar wa Lillaahi’l-hamd (Allaah ni Mkubwa kabisa ….hakuna Mungu isipokuwa Allaah, Allaah ni Mkubwa kabisa, na sifa zote njema ni za Allaah)’. Ibn Abi Shaybah aliripoti haya mahala pengine katika isnaad hiyo hiyo, lakini ikiwa na pamoja na maneno “Allaahu Akbar” ikirejewa mara tatu.
Al-Muhaamili pia ameripoti kuwa Ibn Mas’uud alikuwa akisema : “Allaahu Akbar kabiyran, Allaahu Akbar kabiyran, Allaahu Akbar wa ajall, Allaahu Akbar wa Lillaahi’l-hamd (Allaah ni Mkumbwa kabisa, Allaah ni Mkubwa kabisa, Allaah ni Mkubwa kabisa, Allaah ni Mkubwa kabisa na Mtukufu, na sifa zote njema ni za Allaah)”. (al-Irwaa’, 3/126).
Kupongezana
Watu wanaweza kupeana pongezi na Salaam njema za ‘Iyd, bila ya kujali aina ya maneno. Mfano wanaweza wakaambizana, “Taqabbal Allaah Minnaa Wa Minkum (Allaah Azikubali [Swawm na ibada] zetu na zenu” au “‘Iyd Mubaarak” na mfano wa hayo katika Salaam zilizoruhusiwa.
Tendo la kupeana Salaam limekuwa maarufu wakati wa Maswahaaba na wanavyuoni kama Imaam Ahmad na wengine wameruhusu hilo. Kuna ripoti zinazoonyesha imeruhusiwa kuwapongeza watu katika matukio maalum. Maswahaba walikuwa wakipongezana wakati linapotokea jambo zuri, mfano pale Allaah Alipokubali toba ya mtu n.k.
Hakuna shaka kuwa kumpongeza mtu kwa namna hii ni moja kati ya namna ya heshima zaidi katika tabia njema na ni moja kati ya muamala mzuri sana wa jamii ya Waislam.
Kuvaa Vizuri Zaidi Siku Ya 'Iyd
'Abdullaah bin 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, 'Umar alichagua jubbah (nguo refu inayovaliwa juu ya kanzu) ambayo ilitengenezwa kwa hariri na ilikuwa ikiuzwa kwa bei ya takhfifu sokoni, aliileta kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akasema, "ewe Mtume nunua hii na uvae kwa ajili ya ‘Iyd na watakapokuja wageni" Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema "Hizi ni nguo za yule ambaye hana sehemu akhera (imeripotiwa na Al-Bukhaariy 948)
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikubaliana na mawazo ya ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ya mtu kuvaa vizuri zaidi, lakini alikataa na kupingana na mawazo ya kununua jubbah hilo kwa sababu lilikuwa limetengenezwa kwa hariri.
Al-Bayhaqiy ameripoti kuwa Ibn ‘Umar alikuwa akivaa nguo zake nzuri siku ya ‘Iyd, kwa hivyo wanaume wanatakiwa wavae nguo nzuri zaidi walizokuwa nazo wanapotoka kwa ajili ya ‘Iyd.
Kwa upande mwengine, wanawake, wajiepushe na mapambo wanapotoka kwa ajili ya ‘Iyd, kwa sababu wao wamekatazwa kuonyesha mapambo yao mbele ya wanaume wasio mahrim (wasio na uhusiano nao wa damu) zao. Mwanamke anayetaka kutoka ameharamishiwa kujitia manukato au kujionyesha kwa njia ya kushawishi mbele ya wanaume, kwa sababu yeye ametoka kwa ajili ya ibada tu. Je, unafikiria kuwa ni sahihi kwa mwanamke muumini kumuasi Yule Ambaye yeye (mwanamke) anatoka kwenda kumuabudu, na kwenda kinyume na amri Zake kwa kuvaa nguo za kuvutia zenye kumbana na za rangi zinazong’ara au kujitia manukano n.k?
Shari'ah Katika Kusikiliza Khutba Za 'Iyd
Ibn Qudaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema katika kitabu chake cha al-Kaafi (uk.234):
Imaam anapotoa Salaam (mwisho wa Swalah) atoe khutba sehemu mbili kama khutbah ya Ijumaa kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya hivyo. Khutba ya ‘Iyd ni tofauti na khutbah ya Ijumaa kwa mambo manne, jambo la nne ambali ni Sunnah na sio fardhi kusikiliza kwa sababu imeripotiwa kwamba 'Abdulla bin Al-Saa'ib alisema, "Nilihudhuria ‘Iyd na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alipomaliza kuswali, alisema "tutatoa khutbah sasa kwa hiyo anayependa kukaa (na kusikiliza) akae na yeyote anayetaka kuondoka basi na aondoke".
Katika al-Sharh al-Mumti’ ‘ala Zaad al-Mustanfi’ cha Ibn ‘Uthaymiin, 5/192, kinasema:
“Maneno [ya Ibn Qudaamah], ‘kama khutbah mbili za Ijumaa’ inamaanisha kuwa anatakiwa atoe khutbah mbili, hata kama kuna kutokubaliana katika jambo hili, kama ambavyo tumetaja hapo juu. Khutbah ya ‘Iyd, imeegemea katika shari'ah zilizo sawa na za Ijumaa, hata katika nukta ya kuzungumza wakati wa khutbah hiyo ni haraam, lakini sio wajibu kuhudhuria, hali ya kuwa kuhudhuria khutbah ya Ijumaa ni wajibu, kwa sababu Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala)) Amesema:
"Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Swalah siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara" Al-Jumu'aah :9
Kuhudhuria khutbah ya ‘Iyd sio wajibu, na mtu anaruhusiwa kuondoka, bali iwapo atabakia, ni lazima asizungumze na yeyote. Hivi ndivyo muandishi alivyokusudia aliposema ‘kama khutba mbili za Ijumaa’. “
Mmoja wa wanavyuoni amesema: “Si wajibu kusikiliza khutba za ‘Iyd, kwa sababu kama ingelikuwa ni wajibu kuzihudhuria na kuzisikiliza basi ingekuwa ni haraam kuondoka. Lakini kwa kuwa imeruhusiwa kuondoka, basi si wajibu kusikiliza”.
Hata hivyo, iwapo mazungumzo yatawakera wale wanaosikiliza, ni haraam kuzungumza kwa sababu ya kero hizo, sio kwa sababu ya kutokusikiliza. Kwa msingi huu, iwapo mtu atakuwa na kitabu wakati Imaam anakhutubia, basi ameruhusiwa kukisoma, kwa sababu kufanya hivyo hakutomkera yeyote.
Mtu Kutoka Kwa Njia Moja Na Kurudi Kwa Kutumia Njia Nyengine
Jaabir bin ‘Abd-Allaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameripoti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akibadilisha njia siku ya ‘Iyd. (imeripotiwa na al-Bukhari, 986)
Imeripotiwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitoka kwa miguu, na alikuwa akiswali bila ya adhana wala iqaamah, kisha hurudi kwa kutumia njia nyengine tofauti. Inasemekana kuwa njia hizi mbili zitamtolea ushahidi siku ya Qiyaamah, kwa sababu siku hiyo ardhi itasema juu ya kila kitu kilichofanywa juu yake, zuri na baya. Vile vile inasemekana kuwa imefanywa hivi ili kuonyesha alama na utamaduni wa Kiislam katika njia zote mbili; kutoa ukumbusho wa Allaah; kuwavunja moyo wanafiki na Mayahudi na kuwaogopesha kwa wingi wa watu walio pamoja nae; kutimiza mahitaji wa watu kwa kuwapa fatwa, kuwasomesha na kuwawekea mifano ya kuifuata; kuwapa sadaka wale wanaohitajia; au kuwatembelea jamaa zake na kukuza mahusiano yao.
Tahadhari Juu Ya Kufanya Maovu
Baadhi ya watu wanadhani kuwa Uislam unatuambia kukesha na kuswali usiku wa ‘Iyd, kwa kunakili hadiyth ya uongo inayosema "Yeyote atakayekesha usiku wa ‘Iyd moyo wake hautokufa siku ya kufa moyo wake" Hadiyth hii imeripotiwa katika isnaad mbili moja ambayo ni dhaifu na ya pili ni dhaifu sana. Uislam hautuambii kuutenga usiku wa ‘Iyd kwa kukesha na kusali; hata hivyo, iwapo mtu ana tabia ya kuamka na kusali usiku (Qiyaam), hakuna ubaya wa kufanya hivyo katika usiku wa ‘Iyd pia.
Mchanganyiko wa wanawake na wanaume katika maeneo ya Swalah, mitaani, n.k. Inasikitisha kuwa haya yanatokea sio misikitini tu, bali hata katika sehemu tukufu zaidi, al-Masjid al-Haram [Makkah]. Wanawake wengi, Allaah Awaongoze wanatoka wakiwa hawajajisitiri, wamejipamba na kujitia manukato, wanaonyesha mapambo yao, wakati kuna mkusanyiko mkubwa katika msikiti huo. Hatari ya hali hii iko wazi kabisa. Kwa hiyo wale wahusika ni lazima wapange Swalah za ‘Iyd vizuri, kwa kuweka milango tofauti na njia tofauti kwa wanawake na wawacheleweshe wanaume kutoka mpaka wanawake wawe wameshatoka.
Baadhi ya watu wanajikusanya siku ya ‘Iyd kwa ajili ya kuimba na kufanya aina nyengine za ….burudani, na hii haikuruhusiwa.
Baadhi ya watu wanashereheka katika ‘Iyd kwa sababu Ramadhaan imemalizika na kuwa hawahitajiki tena kufunga. Haya ni makosa, waumini wanasherehekea ‘Iyd kwa sababu Allaah Amewasaidia wao kumaliza mwezi wa Swawm, sio kwa sababu ya kumalizika kwa Swawm ambayo watu wengine wanaichukulia kuwa ni mzigo.
Tunamuomba Allaah Azikubali ibada zetu na toba zetu. Allaah Ampe rehma Mtume wetu Muhammad.