Sunday, December 23, 2012

WAASI WA MJI MWINGINE KATIKA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesema wameuteka mji mwingine katika harakati zao za kuingia katika mji mkuu Bangui, licha ya miito ya viongozi wa kanda kuwataka wasitishe harakati zao za kusonga mbele na kukubali mazungumzo ya amani. Waasi hao wamesema miito ya kufanywa mazungumzo ni sababu nyingine kwa Rais Fancois Bozize, ambaye alitwaa madaraka kupitia mapinduzi ya mwaka wa 2003, kujipa muda zaidi na kuendelea kun'gan'gania madaraka. Taarifa ya waasi hao imesema watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati hawana muda wa kusubiri, na hivyo basi lengo lao ni kumwondoa madarakani kwa nguvu rais Bozize, au kupitia mazungumz. Waasi hao wameiteka miji tisa katika kipindi cha wiki mbili katika harakti zao za kuelekea mji mkuu, ikiwa ni pamoja na mji wa madini ya almasi wa Bria, baada ya kuwazidi nguvu wanajeshi wa serikali. Taarifa iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa muungano wa waasi Justin Mambissi Matar, imesema wameudhibiti mji wa Ippy karibu kilomita 500 kutoka mji mkuu. Mchanganyiko wa uasi ndani ya nchi, machafuko ya kikabila, na migogoro katika nchi jirani za Chad, Sudan na Jamhuri ya Kideomkrasi ya Congo vimehujumu juhudi za kurejesha utulivu katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na utawala mbaya tokea ijipatie uhuru wake hapo mwaka wa 1960.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO