Sunday, January 27, 2013

IRAN KUTOZIUZIA MAFUTA NA GESI BAADHI YA NCHI

Msemaji wa Wizara ya Mafuta nchini Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeamua kusimamisha kuziuzia mafuta ghafi na gesi baadhi ya nchi za Ulaya baada ya nchi hizo kuchukua hatua za kindumakuwili dhidi ya taifa hili. Ali Nikzad amesema kuwa, vikwazo hivyo vya Tehran dhidi ya nchi hizo za Ulaya, vinakuja sambamba na kuongezeka usafirishaji wa mafuta na gesi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuelekea nchi tofauti  za dunia na kwamba, nchi 27 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya zimepigwa marufuku na Tehran kununua bidhaa hiyo muhimu. Aidha akiashiria kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mzalishaji wa pili wa mafuta katika Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani OPEC Nikzad amesema, Iran imechukua hatua hiyo dhidi ya baadhi ya nchi za Ulaya kufuatia kupitishwa kwa duru ya pili ya vikwazo vya mafuta na gesi dhidi yake. Amesema kuwa, vikwazo hivyo vya Tehran dhidi ya nchi hizo za Ulaya vitaendelea hadi pale umoja huo utakapoachana na siasa zake za kiuadui na kubadilisha miamala yake ya kijuba dhidi Iran.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO