Harakati za makundi ya wanamgambo wa Libya zimeendelea kusababisha matatizo chungu mzima ya kiusalama na kuzusha matatizo mengi ya kisiasa nchini humo.
Zimepita siku mbili sasa ambapo wanamgambo wenye silaha wanazingira bunge la nchi hiyo huku wakitoa wito wa kufukuzwa kazi Waziri wa Mambo ya Ndani. Sababu ya kutolewa wito huo ni hatua ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya ya kuanza kutekeleza mpango wa kuwaunganisha wanamapinduzi na makundi ya wanamgambo katika vituo vya polisi na kuvunja kamati za muda za masuala ya usalama. Makundi ya wanamgambo wa Libya yanataka kubakishwa kamati za muda za masuala ya usalama ili ziendelea kufanya kazi na taasisi nyingine rasmi nchini humo. Hata hivyo ukweli wa mambo ni kuwa utendaji kazi wa kamati hizo sambamba na taasisi nyingine za serikali ni moja ya sababu za ukosefu wa amani nchini Libya.
Silaha nyingi zilizotumika katika mapinduzi ya dikteta wa zamani wa Libya zingali mikononi mwa makundi ya wanamapinduzi na wapiganaji wa kikabila. Suala hili la kuwepo maelfu ya silaha mikononi mwa raia linahesabiwa kuwa moja ya changamoto kubwa za usalama na amani nchini Libya. Hii ni kwa sababu, katika miezi ya hivi karibuni kumeripotiwa machafuko na mapigano katika miji mingi ya Libya kati ya makundi ya wanamgambo na askari usalama wa serikali ya nchi hiyo. Makundi hayo yamekuwa yakitumia silaha hizo mara kwa mara kwa ajili ya kuishinikiza serikali ili itekeleze matakwa yao. Wakati huo huo makundi yenye uhusiano na serikali iliyong'olewa madarakani yamekuwa yakitumia vibaya hali hiyo kwa ajili ya kuzusha machafuko na hata kupenya na kuingia katika kamati za kiusalama.
Kwa sasa wanamapinduzi karibu elfu 50 wanahudumu katika kamati za muda za usalama zilizoundwa baada ya kung'olewa madarakani serikali ya Muammar Gaddafi kwa shabaha ya kulinda amani nchini Libya. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa katika kipindi hiki cha kuundwa serikali na utawala mpya nchini Libya kuna udharura wa kuvunjwa makundi yote ya wanamgambo na kuunganishwa katika taasisi moja rasmi. Hata hivyo makundi hayo ya wanamgambo yanapinga suala hilo.
Kwa sasa Libya imetumbukia katika vita vya kuwania madaraka kati ya watawala wa sasa wa nchi hiyo, makundi ya wanamgambo na viongozi wa makabila mbalimbali ya nchi hiyo. Kila mmoja kati ya pande hizo tatu pia hauko tayari kuwa chini ya mwenzake. Japokuwa suala hilo linarejea katika muundo wa kikabila wa nchi hiyo lakini suala ambalo haliwei kupingwa ni kuwa Walibya hawana ada ya kuheshimu sheria. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kwa miaka mingi watu wa Libya hawakufunzwa au kutayarishiwa mazingira ya kuishi ndani ya utawala wa sheria.
Kwa kipindi cha zaidi ya miongo minne Libya ilikuwa ikitawaliwa kwa mujibu wa mfumo makhsusi uliobuniwa na fikra alili za dikteta wa zamani wa nchi hiyo Muammar Ghaddafi. Katika kipindi hicho chote Libya haikuwa na katiba makhsusi inayoakisi matakwa ya Walibya wote. Kwa msingi huo ni jambo la kawaida kuwa watu wa nchi hiyo hawatakuwa na ada au utamaduni wa kufuata na kuheshimu utawala wa sheria. Sehemu kubwa ya Walibya wamezoeshwa kuendesha mambo yako kwa msukumo wa taasubi na jazbaza za kikabila na katika mazingira kama hayo silaha huwa wenzo muhimu wa kufikia malengo na matakwa ya watu.
Matokeo ya hali kama hiyo ni kushadidi ghasia na machafuko ambayo iwapo hayatadhibitiwa Libya inaweza kutumbukia katika dimbwi la matukio machungu na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO