Monday, January 21, 2013

MAZOEZI YA KIJESHI YA RUSSIA NI UJUMBE KWA NCHI ZA MAGHARIBI

Majeshi ya Russia kuanzia siku ya Jumapili ya tarehe 20 Januari yanafanya manuva makubwa ya kijeshi ya baharini ambayo hayajawahi kuonekana katika muongo mmoja wa hivi karibuni. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia amesema kuwa, lengo la manuva hayo ni kuandaa komandi za kijeshi na hali kadhalika kuvipa mazoezi ya kutosha vikosi vya majini katika kutekeleza operesheni kwenye maji ya mbali. Msemaji huyo ameongeza kuwa, luteka hiyo inazishirikisha manowari za kijeshi zilizoko kaskazini mwa Russia, manowari zilizoko eneo la Baltic, Komandi ya Nne ya ulinzi wa anga na  jeshi la anga la nchi hiyo. Amesema kuwa, manuva hayo yaliyoanza tarehe 20 yataendelea hadi tarehe 29 Januari kwa kuzishirikisha manowari kubwa nane za kivita, meli zinazoshambulia nyambizi na meli kadhaa za kutoa misaada. Imeelezwa kuwa, manuva hayo ya siku kumi yanafanyika zaidi katika eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterranean yaani kwenye mpaka wa majini wa Syria na bandari ya Tartus ya nchini humo. 
Manuva ya Russia ni ujumbe mzito na wa wazi kwa nchi za Magharibi ambazo zinafanya juhudi za kutaka kuingia kijeshi kwenye mgogoro wa Syria. Nchi za Magharibi hivi sasa zimeanzisha mashambulizi kusini mwa bahari hiyo katika eneo la kaskazini na magharibi mwa Afrika.  Bahari ya Mediterranean ilikuwa na nafasi muhimu kwa nchi za Nato wakati zilipoishambulia kijeshi Libya. Hivi sasa Ufaransa kwa kuanzisha mashambulizi yake nchini Mali, imekuwa na nafasi muhimu pia katika kupitishia kwenye bahari hiyo zana zake za kijeshi kuelekea nchi za Kiafrika. Bahari ya Mediterrannean siku hadi siku inazidi kuwa na umuhimu wa kiistratijia kutokana na mgogoro unaoendelea kutokota nchini Syria. Nchi za Magharibi katika miezi ya hivi karibuni zimekuwa zikifanya njama kubwa za kuandaa mazingira ya kutumiwa nguvu za kijeshi dhidi ya Syria. Kuwekwa makombora ya Patriotic katika mpaka wa Uturuki na Syria ni miongoni mwa uingiliaji kati huo wa nchi za Magharibi. Warussia wanasimama kidete na kukabiliana vikali na njama za wapinzani wake wa Magharibi za kutaka kubadilisha kwa mabavu tawala zisizoziunga mkono nchi za Magharibi, ukiwemo utawala wa Rais Bashar Assad wa Syria. Serikali ya Moscow imeonyesha kuwa tayari kijeshi kwa kufanya manuva ya kijeshi ili kuonyesha ungangari wake dhidi ya Wamagharibi. Miaka miwili iliyopita katika kuonyesha radiamali yake juu ya kuongezeka harakati za manowari za kivita za Nato katika bahari hiyo, Russia ilituma manuwari zake ikiwemo ile inayobeba ndege zenye makombora ya nyuklia. Ni wazi kuwa kwa kushadidi hivi karibuni harakati za manowari za kijeshi za Russia katika bandari ya Tartus, ambapo imekuwa ikiitumia kama kituo cha kijeshi tokea kipindi cha Umoja wa Kisovieti, nchi hiyo inataka kuthibitisha kuwa haiko tayari kuwapatia mwanya washindani wake wa Magharibi katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO