Monday, January 21, 2013

VITISHO VYA ISRAEL DHIDI YA MASJID AQSAA VYAONGEZEKA

Vitisho vya Wazayuni dhidi ya msikiti wa al Aqsa bado vinaendelea, na mara hii mjumbe wa chama kinachoitwa "Yisrael Beiteinu” ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel kuuripua msikiti huo. Matamshi hayo ya Wazayuni waliofurutu ada yanaonyesha ukubwa wa hatari ya njama za Wazayuni dhidi ya msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu. Hii ni katika hali ambayo Pair Lepid, mkuu wa chama kingine cha Kizayuni ambacho kinaunga mkono pia siasa za kupenda kijipanua za utawala haramu wa Israel amekosa haya na wala soni usoni na kuthubutu kutangaza kuwa, Quds utakuwa mji mkuu wa utawala huo haramu. Matamshi hayo yanatolewa katika hali ambayo, Avigdor Lieberman, waziri wa zamani wa mashauri ya kigeni wa Israel pia amesisitiza juu ya kupanuliwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hasa kwenye mji wa Baitul Muqaddas. Kwa ujumla matamshi hayo ya viongozi wa utawala wa Kizayuni yanabainisha kuendelea malengo yao ya uharibifu dhidi ya msikiti wa al Aqsa na pia harakati zao za kutaka kuudhibiti mji wa Baitul Muqaddas. Hila na kuongezeka vitishio mbalimbali vya Wazayuni dhidi ya msikiti huo, kunadhihirisha suala hili kwamba, njama za Israel dhidi ya msikiti huo zimeingia katika kipindi cha hatari zaidi na kuna uwezekano wa kutekelezwa mipango miovu ya utawala huo ya kutaka kukiharibu kikamilifu kibla hicho cha kwanza cha Waislamu. Wazayuni wanatumia njia tofauti za kuuharibu msikiti wa al Aqsa ikiwa ni pamoja na kuchimba mashimo mengi na njia za chini ya msikiti huo mtukufu na kando kando yake. Vitendo hivyo kwa kweli vina lengo la kuzidhoofisha kuta za msikiti wa al Aqsa ili eneo hilo takatifu liweze kuharibika kikamilifu kwa mtikisiko mdogo tu wa ardhi au mripuko. Miezi kadhaa iliyopita, Wazayuni wenye misimamo mikali wakiwa na lengo la kuiandalia mazingira Israel ya kuharibu msikiti wa al Aqsa, walichapisha picha za mji wa Baitul Muqaddas huku msikiti huo ukiwa haupo. Hivi karibuni pia ilifichuliwa kuwa, moja ya mashirika ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni linalojulikana kwa jina la 'Kaj" lilifanya kikao na marubani wa Kizayuni kuwashawishi wadodoshe bomu kwenye msikiti huo. Inaelezwa pia kuwa, kimefanyika kikao kati ya makamanda wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada, kwa ajili ya kutayarisha mashambulizi ya kuharibu msikiti wa al Aqsa. Tangu kuundwa utawala huo pandikizi katika ardhi za Palestina hadi hivi sasa, msikiti mtukufu wa al Aqsa umeshashambuliwa mara kadhaa na Wazayuni. Mwaka 1969 Wazayuni wenye misimamo mikali wakiongozwa na Dennis Michael Rohan waliuchoma moto msikiti huo wa kihistoria wa al Aqsa, hatua ambayo iliratibiwa na makundi ya watalii kwa ushirikiano na viongozi wa Tel Aviv. Katika tukio hilo chungu, mita mraba zisizopungua 200 za dari ya msikiti huo ziliharibiwa na kuanguka kabisa, pande tano za kuba la msikiti huo ziliungua na mimbari yenye thamani kubwa iliyojengwa miaka 800 iliyopita iliteketea kabisa kwa moto. Huku mji wa Baitul Muqaddas na msikiti wa al Aqsa ukikabiliwa na duru mpya ya vitisho na njama za utawala wa Kizayuni, fikra za walio wengi duniani wanaitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti na za haraka za kupambana na utawala huo usio na chembe ya ubinadamu wakiamini kwamba, kucheleweshwa suala hilo kutaifanya Israel iendelee na hatua zake hizo za uharibifu bila ya woga.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO