Saturday, January 19, 2013

UFARANSA YAOMBA MSAADA KUIKABILI MALI

Ufaransa imeomba msaada kwa serikali ya Canada kwa ajili ya kuingilia zaidi kijeshi nchini Mali. Hayo yameandikwa na mtandao wa gazeti la Ufaransa wa Le Figaro ukimnukuu balozi wa Ufaransa mjini Ottawa, Canada alipokutana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo John Bird na kusisitiza kwamba, Paris inahitaji msaada wa Canada kwa ajili ya kuwasafirisha askari wake huko nchini Mali kwa ajili ya kuendelea na oparesheni zake za kijeshi ilizozianzisha katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Aidha Ufaransa imetaka kupewa na Canada ndege za kijeshi aina ya C 17 iweze kuzitumia kwa kipindi kisichojulikana. Siku ya Jumatano Waziri Mkuu wa Canada Stephen Joseph Harper alifanya mazungumzo ya simu na Rais François Hollande wa Ufaransa kuhusiana na uingiliaji wa kijeshi nchini Mali na kusisitiza kwamba, serikali ya Ottawa haiko tayari kuingilia mgogoro wa nchini Mali pamoja na kwamba, inaunga mkono operesheni hizo za kijeshi. Hadi jana, Ufaransa ilikuwa tayari imetuma askari wake 1400 nchini Mali. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba, Paris inajitahidi kuzishawishi nchi nyingine kuingilia mgogoro wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, ili isibakie peke yake katika kile linachoonekana ni kinamasi ilichotumbukia Ufaransa huko nchini Mali.
WANAJESHI WA UFARANSA PAMOJA NA WA UINGEREZA WAKIWA NJIANI KUELEKEA BAMAKO

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO