Tuesday, January 01, 2013

WAISLAM UFARANSA WAZIDI KUNYANYASWA

Waislamu wenye asili ya Morocco katika mji wa Bordeaux kusini mwa Ufaransa, hivi karibuni wamekumbana na zahama na chachawizo nyingine baada ya sehemu waitumiayo kwa ajili ya kufanyia ibada ya sala kushambuliwa na watu wasiojulikana. Hii ni mara ya nne kwa sehemu hiyo iliyoko katika eneo la kusini magharibi mwa Ufaransa, kushambuliwa na watu wasiojulikana. Kabla ya hapo, kuta za jengo hilo ziliwahi kuandikwa nara za kibaguzi na chuki dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu. Kila mara kumekuwa kukisikika na kushuhudiwa vitendo vya uchomwaji moto misikiti na maeneo mengine ya ibada ya Waislamu, kusambazwa na kuchapwa vikatuni vinavyoyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu kwenye magazeti ya nchi hiyo pamoja na kuwekwa sheria ngumu na kali dhidi ya wanawake wa Kiislamu wanaovaa vazi la hijabu. Waislamu walio wengi nchini Ufaransa ni wahajiri kutoka nchi za Algeria, Morocco, Tunisia na nchi nyingine za magharibi mwa Afrika zilizokoloniwa na nchi hiyo. Dini ya Kiislamu inahesabiwa kuwa dini ya pili kwa ukubwa nchini Ufaransa, baada ya dini ya Kikristo. Licha ya Waislamu kulalamikia ongezeko la vitendo vya ukandamizaji, unyanyasaji na uvunjiwaji heshima matukufu ya Kiislamu, amma hadi sasa bado haijasikika ripoti yoyote kutoka kwa viongozi wa Ufaransa inayoelezea kuadhibiwa watenda jinai hizo. Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu cha Ufaransa tarehe 3 mwezi huu wa Disemba kilitoa taarifa na kueleza kuwa, vitendo vya kiadui dhidi ya Waislamu mwaka huu 2012, viliongezeka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na miaka iliyopita. Ripoti hiyo pia imeashiria vitendo kadhaa vya vitisho dhidi ya Waislamu vikiwemo vya kupigwa, uchomwaji moto, kuharibiwa mali na kuvunjiwa heshima matukufu ya Waislamu, kwa lengo la kuharibu sura ya dini ya Kiislamu kati ya wananchi wa nchi hiyo. Gazeti la Kifaransa la Le Figaro liliandika katika ripoti yake ya mwezi Novemba juu ya wasiwasi wa kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya dini ya Kiislamu nchini Ufaransa katika miezi kumi ya awali ya mwaka huu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu mwaka 2011 vilikuwa 123, katika hali ambayo katika kipindi cha miezi 10 tu ya awali ya mwaka huu vilifikia 175. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na French Institute of Public Opinion IFOP, mitazamo ya wananchi wa Ufaransa kuhusiana na Waislamu imekuwa mibaya zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Taarifa zinasema kuwa, mwezi Oktoba uliopita, karibu Wafaransa 70 walio na chuki na Uislamu, walikusanyika katika eneo linalojengwa msikiti katika mji mmoja ulioko katikati mwa Ufaransa na kuwashambulia wajenzi wa msikiti huo. Mwezi Novemba mwaka huu pia, mamia ya Wafaransa wenye fikra za utaifa walifanya maandamano katika mji wa Paris, na kupiga nara dhidi ya siasa za serikali ya nchi hiyo za kuwapokea Waislamu katika jamii ya Wafaransa. Waandamanaji hao waliitaka serikali kutekeleza siasa za kuwafukuza Waislamu na wageni katika nchi za Ulaya. 

Waislamu wa Ufaransa wanaofikia zaidi ya milioni tano na kuhesabiwa kuwa idadi kubwa zaidi ya wafuasi wa dini hiyo tukufu barani Ulaya, hawana haki zozote za maana wakilinganishwa na raia wengine wa nchi hiyo; na serikali ya Paris imekataa katakata kutoa walau kiti kimoja  cha uwakilishi wa jamii ya Waislamu katika bunge la nchi hiyo. Wajumbe wa Baraza la Waislamu la Ufaransa mara kadhaa wameelezea wasiwasi wao dhidi ya wimbi la vitendo vya uadui dhidi ya dini ya Kiislamu nchini humo na wamewataka viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo kuingilia kati na kuondosha vitendo hivyo vya kiadui. Wajumbe wa baraza hilo wamewahi kukutana na Rais François Hollande na Jean-Marc Ayrault Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kuwataka wakabiliane na vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu kama wanavyofanya kuhusiana na Mayahudi nchini humo, lakini bila ya mafanikio yoyote.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO