Harakati ya Mapambano ya Hizbullah kwa kushirikiana na Harakati ya Amal zote za Lebanon, zimetangaza kuwa tayari kikamilifu kukabiliana na hujuma yoyote ya kiuadui inayoweza kufanywa na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya taifa hilo. Viongozi wa harakati ya Amal na Hizbullah waliyasema hayo siku ya Jumamosi usiku, katika ripoti ya pamoja na kusisitiza kuwa, harakazi hizo zipo tayari kikamilifu kwa ajili ya kulinda taifa, ardhi na izza ya Lebanona kutokana na aina yoyote ya hatua ya kiuendawazimu ya Wazayuni na kwamba, ikiwa Israel itathubutu kuanzisha chokochoko dhidi ya taifa hilo, basi zitatoa jibu kali kwa vitisho vya utawala huo. Hayo yamejiri kufuatia hatua ya Israel ya kuongeza idadi ya askari wake katika mpaka wake wa pamoja na Lebanon sambamba na kuongeza vitisho dhidi ya taifa hilo la Kiarabu. Sambamba na ripoti ya kulaani hatua hiyo ya Israel ya kuongeza askari wake katika maeneo yaliyotajwa na kuongezeka kwa hatua za kichokozi za mara kwa mara kama vile kukiuka anga, ardhi na bahari ya Lebanon, harakati hizo zimeitaka pia serikali ya Bairut kuchukua hatua kali zitakazosaidia kukomesha uchokozi huo wa Wazayuni. Aidha jeshi la Lebanon pia limetoa ripoti ya kulaani hatua hizo za Wazayuni katika maeneo ya mpakani na kusisitiza kuwa, jeshi hilo limejiandaa vilivyo kwa ajili ya kukabiliana na uchokozi wowote wa Israel. Ripoti za vyombo vya kiintelijensia na usalama nchini Lebanon zinaonyesha kuwa, katika siku chache zilizopita utawala wa Kizayuni umeweka mamia ya askari wake na makumi ya magari ya deraya katika maeneo ya mpakani hususan katika eneo la Shab'aa huku helikopta na ndege za upelelezi za utawala huo zikionekana katika anga ya maeneo ya Jolan na Shab'aa. Hii ni katika hali ambayo Aizenberg kamanda wa usalama wa ndani wa jeshi la Israelamekiri kwamba, ikiwa kutazuka vita vipya kati ya utawala huo na Lebanon, basi vita hivyo vitailetea hasara kubwa Israel kuliko hasara iliyoipata katika vita vya mwaka 2006. Kamanda huyo ametabiri kuwa, ikiwa utawala huo utaingia katika vita vipya na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon, kuna uwezekano harakati hiyo ikavurumisha makombora yake kuelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, mara kumi zaidi ya makombora yaliyovurumishwa katika vita vya mwaka 2006. Itakumbukwa kuwa, Israel ilishindwa vibaya na Hizbullah katika vita vya siku 33 mwaka mwaka huo na kulazimika kutoka katika maeneo ya kusini ya Lebanon baada ya kukubali azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililoutaka utawala huo kuheshimu anga na ardhi ya Lebanona. Hata hivyo tokea wakati huo Israel imekuwa ikikiuka azimio hilo mara kwa mara kwa kudumisha hatua zake za kichochezi na kichokozi dhidi ya Lebanon.
Na Sudi Jaafar Shaaban
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO