Thursday, February 28, 2013

ISRAEL YAZIDI KUSAKAMWA KUTOKANA NA MATESO YAKE KWA WAPALESTINA

Kushadidi jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina katika magereza ya utawala huo usio na utu wala chembe ya ubinaadamu kumewafanya mateka madhulumu wa Kipalestina wakabiliwe na kifo cha polepole. Lakini walimwengu ni wanadamu, jinai hizo za Wazayuni zimewafanya walimwengu kutoka kila kona ya dunia kulaani vikali jinai hizo. Malalamiko ya walimwengu yamechukua wigo mpana zaidi baada ya kufa shahidi mateka wa Kipalestina Arafat Jaradat. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa tena huru kuhusiana na kifo cha mateka huyo wa Kipalestina. Kuhusiana na suala hilo, Robert Serry, Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Mashariki ya Kati ametaka kuundwe kamati huru ya kutafuta ukweli ambayo itakuwa na jukumu la kuchunguza namna Mpalestina huyo alivyofariki dunia. Amesisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa kutokana na kuzidi kuwa mbaya hali ya mateka wa Kipalestina katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel. 
Hii ni katika hali ambayo, Wasil Abu Yusuf, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO amesema kuwa, Wapalestina watawasilisha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ili kuzuia ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina unaofanyika kila uchao katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Kwa upande wake, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imetoa taarifa na kulaani vikali kuuawa Arafat Jaradat, mateka wa Kipalestina. Profesa Ekmeleddin Ihsanoğlu, Katibu Mkuu wa OIC amelaani kitendo cha Wazayuni cha kumuua shahidi Jaradat na kusema kuwa, kitendo hicho ni jinai ya wazi na ukiukaji wa dhahiri kabisa wa haki za kimataifa. Amesema, kifo cha Jadarat kimefichua tena jinai na siasa za kibaguzi za Israel. Katibu Mkuu wa OIC amezitaka asasi za kimataifa kuwa amilifu zaidi katika hili na kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel ili uachane na siasa zake za muamala mbaya na mateso dhidi ya wafungwa wa Kipalestina na uwaachilie huru mara moja mateka hao wa Kipalestina unaowashikilia katika magereza yake ya kutisha. Kadhalika wananchi wa Palestina walijitokeza kwa wingi katika shughuli ya maziko ya Arafat Jaradat na kusisitiza kwamba, damu ya shahidi hiyo haitapotea bure. Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kwamba, kutokana na kutanda wingu zito la malamiko na upinzani wa Wapalestina dhidi ya Wazayuni, ni ishara ya kuingia Intifadha ya wananchi wa Palestina katika marhala mpya. Viongozi kadhaa wa nchi za Kiarabu na Kiislamu pia wametoa taarifa kwa nyakati tofauti wakilaani siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu imetoa taarifa maalumu ambapo sambamba na kulaani jinai hiyo ya Israel imesisitiza kwamba, kitendo hicho cha Israel ni ukiukaji wa wazi kabisa wa haki za binadamu. Iran imezitaka asasi za kimataifa hususan mashirika ya kutetea haki za binadamu ulimwenguni kuchukua hatua za maana na za kivitendo ili kuzuia kukaririwa maafa ya kibinadamu huko Palestina ambayo ni kinyume kabisa na mikataba ya kimataifa. Hapana shaka kwamba, kimya cha asasi za kieneo na kimataifa kwa jinai za Israel kwa upande mmoja, na uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa Tel Aviv kwa upande wa pili, ni mambo ambayo yamekuwa yakiupa kiburi utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuendeleza jinai zake hususan dhidi ya mateka wasio na ulinzi wa Kipalestina.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO