Wednesday, March 27, 2013

ALSHABAB WAHUSISHWA NA UBAKAJI SOMALIA


Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limewatuhumu wanajeshi wa serikali ya Somalia na kundi la wanamgambo wa Al Shabab kwa kuwabaka na kuwanajisi wakimbizi wanawake walioko kwenye kambi za wakimbizi pambizoni mwa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo imeeleza kuwa, wanawake ambao walikimbilia kwenye kambi hizo wakihofia mashambulizi ya makundi yanayobeba silaha na baa la njaa wamekuwa katika wakati mgumu baada ya kukabiliwa na vitendo vya kikatili vya kubakwa na kunajisiwa na wanamgambo wa kundi la al Shabab pamoja na baadhi ya wanajeshi wa serikali la Somalia. Taarifa hiyo imeeleza kuwa, hali ya wakimbizi hao bado haijaboreka ijapokuwa serikali mpya iliyochukua madarakani mwezi Septemba mwaka uliopita iliahidi kulishughulikia kikamilifu suala hilo. Kundi la al Shabab ambalo linafungamana na mtandao wa al Qaeda linadhibiti baadhi ya maeneo ya katikati na kusini mwa Somalia na limekuwa likivishambulia vikosi vya serikali na vile vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO