Saturday, March 30, 2013

KANISA KATOLIKI LAONYA KUENEA UMASIKINI ULAYA


Makanisa Katoliki ya Ujerumani na Italia yametoa tahadhari ya kuenea umasikini barani Ulaya na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua kwa minajili ya kukabiliana na wimbi la umasikini. Mtandao wa Habari wa al-Masri al-Yaum umeyanukuu makanisa ya Kikatoliki ya Ujerumani na Italia yakisisitiza kwamba, kuna haja kwa serikali barani Ulaya kuwazingatia wananchi wanaokabiliwa na umasikini barani humo. Robert Zollitsch, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani ametangaza kuwa, serikali ya nchi hiyo inapaswa kushughulikia tatizo la umasikini linalowakabili wananchi na kwamba, itazame upya sera zake za ustawi na zile za masuala ya fedha.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani ameongeza kuwa, hali ya umasikini inayowakabili wananchi nchini humo haipasi kuachwa iendelee. Aidha Askofu Robert Zollitsch amevikosoa vyombo vya habari vya Ujerumani kutokana na kutoakisi kwa uwazi habari za umasikini katika nchi hiyo na kusisitiza kwamba, suala la umasikini nchini humo haliripotiwi kama inavyotakiwa. Aidha amesema, umasikini nchini Ujerumani hususan katika miji mikubwa upo katika hali ya kupanuka na kuenea.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO