Rais Hamid Karzai wa Afghanistan leo anatazamiwa kuwa na mazungumzo nchini Qatar juu ya pendekezo la kufunguwa ofisi ya kundi la Taliban katika taifa hilo la Ghuba ikiwa kama ni hatua ya kwanza juu ya uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo ya kukomesha vita vilivyodumu zaidi ya muongo mmoja nchini Afghanistan. Karzai huko nyuma alikuwa amepinga kufunguliwa kwa ofisi hiyo akihofia kuwekwa kando kwa serikali yake katika mazungumzo yoyote yale yatakayowahusisha wanamgambo hao wa itikadi kali na Marekani. Wanamgambo hao wanagoma kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na rais huyo wa Afghanistan kwa kusema kwamba ni kibaraka wa Marekani ambayo ilisaidia kumuweka madarakani baada ya operesheni ya kijeshi ya kuu'gowa utawala wa Taliban kutoka Kabul hapo mwaka 2001. Kutokana na kwamba vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO vinavyoongozwa na Marekani vinatarajiwa kuondoka nchini Afghanistan mwishoni mwa mwaka 2014 Karzai amekubali pendekezo la kuwepo kwa ofisi ya Taliban katika mji mkuu wa Qatar Doha na anatarajiwa kuutaja mpango huo wakati wa mazungumzo yake na Mfalme wa Qatar leo hii.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO