Tuesday, March 26, 2013

MAHAKAMA YA JUU YA KENYA YATAKA KURA KUHESABIWA TENA BAADHI YA VITUO



Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamuru kura zihesabiwe upya katika vituo 22, kufuatia uchaguzi wa urais ambao uliepuka duru ya pili kwa kura chache. Amri iliyotolewa na jaji wa mahakama hiyo hivi leo, Smokin Wanjila, imetaka kuhesabiwa upya kwa kura katika vituo hivyo, ambavyo ni kama chembe tu ya vituo 32,000 vilivyokuwepo katika uchaguzi wa Machi 4, kuanze kesho.
Pia nayo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetakiwa kuweka wazi daftari la wapiga kura ililotumia kuhesabu kura, baada ya mfumo wa elektroniki kukwama. Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yalimpa ushindi Uhuru Kenyatta, ambaye alivuuka mstari wa asilimia 50 kwa kura 8,000 tu.
Hata hivyo, Kenyatta alimzidi mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga, kwa kura 800,000. Muungano wa CORD, unaoongozwa na Odinga, na mashirika kadhaa ya kiraia wamewasilisha kesi katika mahakama ya juu ya Kenya, wakilalamikia kile walichokiita hitilafu kubwa wakati wa uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO