Tuesday, March 26, 2013

RAIS WA ZAMBIA AACHIWA KWA DHAMANA



Rais wa zamani wa Zambia, Rupia Banda ameachiliwa huru kwa dhamana baada ya kukamatwa na kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za ufisadi na utumizi mbaya wa madaraka. Wakili wa Banda, Sakwiba Sikota amesema mteja wake hana hatia na kwamba ana imani mahakama itadhihirisha hilo. Sikota ameongeza kuwa, Banda ataanza kuhudhuria vikao vya mahakama hapo Kesho. Rupia Banda anatuhumiwa kuiba zaidi ya dola milioni 11 kutoka hazina ya taifa katika kipindi cha uongozi wake. Bunge la Zambia mapema mwezi huu lilimuondolea kinga ya kutoshtakiwa na hivyo kutoa fursa kwa polisi kumkamata na kumfungulia mashtaka. Banda amewaambia wafuasi wake nje ya korti kwamba yeye ni raia mwema anayefuata sheria za nchi na amewataka kuwa watulivu huku kesi yake ikiendelea. Banda aliingia madarakani Agosti mwaka 2008 baada ya kufariki dunia, Levy Mwanawasa na kisha kushinda kwenye uchaguzi wa rais miezi miwili baadaye. Alishindwa kutetea wadhifa wake kwenye uchaguzi wa mwaka 2011 aliposhindwa na mpinzani wake wa muda mrefu, Michael Sata.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO