Sunday, March 31, 2013

MAREKANI ITABEBA LAWAMA VITA YA KOREA

Mchambuzi mmoja mwandamizi wa masuala ya kijeshi amesema kuwa, Marekani ndiyo itakayobeba lawama iwapo kutatokea vita kati ya Korea mbili zilizogawanyika. Jeff Steinberg wa jarida la kila wiki la Executive Intelligence Review (EIR) la nchini Marekani ameiambia televisheni ya Press TV kuwa, Marekani ambayo ni dola lenye nguvu duniani inataka kulisukuma mbele suala hilo hadi kuitumbukiza dunia katika vita ambavyo kuna uwezekano vikawa vya nyuklia. Amesema, mpira hauko katika uwanja wa Korea Kaskazini, bali uko kwenye uwanja wa Marekani. Korea Kaskazini imesema kuwa, kuanzia sasa uhusiano wake utakuwa ni wa zama za vita na masuala yote yanayohusiana na Korea mbili yatazingatiwa kwa protokali ya wakati wa vita. Vile vile imeonya kuwa, uchokozi wa aina yoyote ile wa kijeshi karibu na Korea Kaskazini, iwe ni ardhini au kwenye mpaka wa baharini, utashuhudia majibu makali sana na utakuwa mwanzo wa vita vya nyuklia. Hivi karibuni Marekani ilifanya manuva ya kijeshi karibu na Korea Kaskazini ikishirikiana na Korea Kusini hatua ambayo iliikasirisha sana Korea Kaskazini; nchi ambayo inaamini pia kuwa Marekani ilichochea vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa dhidi yake, baada ya Pyongyang kufanya majaribio ya nyuklia mwezi Februari mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO