Thursday, March 28, 2013

SERIKALI YA UINGEREZA YASHINDWA RUFAA YA SHEIKH ABU QATADA


Serikali ya Uingereza kwa mara nyingine imeshindwa kwenye mahakama kuu ya nchi hiyo kwenye rufaa waliyokuwa wamekata wakitaka kurejeshwa nchini Jordan kwa mtuhumiwa wa vitendo vya ugaidi Sheikh, Abu Qatada. Katika hukumu ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na Serikali ya Uingereza, majaji watatu waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyi walijiridhisha na upande wa utetezi ambao uliwasilisha nyaraka zinazoonesha kuwa Abu Qatada akirejeshwa nchini Jordan atafanyiwa vitendo vya unyanyasaji. Katika kufikia uamuzi wao majaji hao wamekataa ombi la Serikali ya Uingereza kutaka kumsafirisha kiongozi huyo wa kidini kwenda nchini Jordan kukabiliana na mashtaka ya ugaidi ambayo yanamkabili.

Ofisi ya wizara ya mambo ndani nchini humo kwenye taarifa iliyoichapisha kwenye mtandao wa Twitter, imesema kuwa bado haijakata tamaa dhidi ya kutaka kumrejesha nchini Jordan kiongozi huyo na kwamba wanajiandaa kuwasilisha ombi jingine la kwanini kiongozi huyo arejeshwe nchini Jordan. Abu Qatada alikamatwa hivi karibuni na maofisa uhamiaji kwenye mpaka wa nchi ya Uingereza na kudai kuwa kiongozi huyo alipanga kutoroka jambo ambalo mawakili wake walilikanusha. Hata hivyo kiongozi huyo kwa mara nyingine ameachiwa kwa dhamana licha ya kukiuka matakwa ya dhamana aliyokuwa amepatiwa hapo awali.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO