Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema natija ya vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran ni kuongeza motisha ya taifa la Iran katika mkondo wa ustawi na maendeleo.
Admeli Habibullah Sayyari ameongeza kuwa nchi za Magharibi zimetumia uwezo wao wote kuishinikiza na kuiwekea vikwazo Iran lakini kwamba haziwezi kufikia natija ya njama zao. Amesema njama za Wamagharibi dhidi ya Iran zimepelekea taifa la Iran kufanya hima katika ustawi wa sayansi, elimu na kujitegemea. Admeli Sayyari amesema kuwepo meli za kivita za Iran katika maji ya kimataifa pamoja na kulinda doria kieneo na kimataifa ni ishara ya uwezo mkubwa wa wanamaji wa Iran. Ameongeza kuwa leo Jeshi la Wanamaji la Iran limeweza kujitegemea kikamilifu katika uga wa ukarabati na utunzaji zana za kivita. Admeli Sayyari pia ameashiria kuanza kutumika meli ya kivita ijulikanayo kama 'Jamaran 2' katika Bahari ya Kaspi kaskazini mwa Iran na kusema pamoja na kuwepo vikwazo vyote vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran katika sekta ya kijeshi, manowari hii ya kisasa kabisa imeanza kazi baada ya kutengenezwa kikamilifu na wataalamu wa hapa nchini.
Manowari ya 'Jamaran 2' ambayo ilikuwa inatarajiwa kuanza kutumika miezi michache ijayo iliweza kuzinduliwa mapema zaidi katika hafla iliyohudhuriwa na Rais Ahmadinejad siku ya Jumapili.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO