Friday, April 12, 2013

AFRIKA KUSINI HAWAMUOOMBOLEZI YA THATCHER

Walio wengi Afrika Kusini wamekataa kuomboleza kifo cha waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Margaret Thatcher kutokana na sera zake potofu za kuunga mkono utawala wa ubaguzi wa rangi na kukitaja kuwa cha 'kigaidi' chama cha ANC kilichopigania ukombozi wa nchi hiyo.
Thatcher ambaye alikuwa waziri mkuu wa Uingereza kuanzia mwaka 1979 hadi 1990 aliaga dunia Jumatatu akiwa na umri wa miaka 87.
Habari za kifo chake hazikuwahuzunisha watu wa Afrika Kusini na wale wote waliokuwa wapinzani wa ubaguzi wa rangi ambao wanasema Thatcher alikuwa mbaguzi. Katika miaka ya 80 wakati utawala wa ubaguzi wa rangi ulipoanza kuwakandamiza wapigania ukombozi wazalendo, Thatcher alipinga vikali juhudi za Jumuiya ya Madola za kuzidisha vikwazo dhidi ya utawala huo uliokuwa ukiongozwa na makaburu walio wachache. Katika matamshi yaliyowakasirisha wengi mwaka 1987, Thatcher alikitaja chama cha ANC cha shujaa Nelson Mandela kuwa ni chama cha kigaidi. Wakati huo Mandela alikuwa gerezani akihudumia kifungo cha miaka 27 kutokana na juhudi zake za kupigania ukombozi. Thatcher pia aliwahi kusema kuwa yeye ni rafiki wa kaburu P.W. Botha aliyekuwa kiongozi katili wa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO