Msikiti mmoja katika kitongoji cha mji mkuu wa Sweden, Stockholm umeruhusiwa
kuadhini kwa kutumia kipaza sauti kilicho kwenye mnara kwa ajili ya Sala ya
Ijumaa. Hii ni mara kwa kwanza kwa nchi hiyo ya Scandinavia kuruhusu adhana kwa
sauti inayosikika nje ya msikiti.
Idara ya polisi mjini Stockholm imesema msikiti huo utaruhusiwa kuadhini kwa
muda wa kati ya dakika tatu na tano katika kipindi cha baina ya saa sita na saa
saba mchana kila Ijumaa. Mkuu wa Jumuiya ya Utamaduni wa Kiislamu katika eneo la
Botkyrka kusini mwa Stockholm Bw. Ismail Okur ameupongeza uamuzi huo. Ombi la
kuadhini kwa sauti inayotoka nje ya msikiti liliwasilishwa miaka mitano
iliyopita. Kuna karibu Waislamu 7,000 katika eneo hilo na aghalabu wana asili ya
Uturuki. Chama chenye chuki dhidi ya Uislamu cha Sweden Democrats kimepinga
uamuzi huo. Katika miaka ya hivi karibuni idadi ya Waislamu barani Ulaya
imeongezeka kwa kasi na sambamba na hilo hitajio la misikiti pia limeongezeka.
Waislamu raia wa nchi za Ulaya wamekuwa wakibaguliwa kwa muda mrefu na sasa
wanapigania haki sawa na raia wengine wa Ulaya.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO