Wednesday, April 03, 2013

IRAN YASEMA MKATABA WA SILAHA NI WA KIBAGUZI


Mwanadiplomasia mwandamizi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani Mkataba Mpya wa Biashara ya Silaha (ATT) uliopasishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusema mkabata huo una malengo ya kisiasa na ni wa kibaguzi.
Akihutubu mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa Bw. Gholam-Hossein Dehqani amesisitiza kuwa katika hali ambayo lengo kuu la ATT ni kudhibiti biashara ya silaha duniani lakini rasimu ya mwisho ya mkataba huo bado inaruhusu kupelekewa silaha vikosi ambavyo haviko katika nchi zao. Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema kutumwa silaha Mashariki ya Kati na eneo la Ghuba ya Uajemi ni jambo ambalo limeathiri vibaya usalama na maisha ya watu wa eneo hilo na kusababisha idadi kubwa ya watu kupoteza maisha. Dehqani amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ilijaribu kurekebisha makosa ya kisheria katika rasimu ya mkataba huo kwani ulitayarishwa 'kwa malengo ya kisiasa'. Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema mkataba huo umeandikwa ili kukidhi matakwa ya Marekani na muitifaki wake mkuu, Israel. Iran imekosoa mkataba huo kwa sababu hauzuii nchi vamizi kuuziwa silaha. Nchi zilizopiga kura dhidi ya ATT ni pamoja na Iran, Syria na Korea Kaskazini huku wauzaji wakubwa wa silaha kama Russia na China zikijizuia kupiga kura pamoja na nchi zingine 20 duniani.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO