Waziri Mkuu wa Malaysia, Najib Razak ametangaza kulivunja bunge ili kutoa fursa ya kufanyika uchaguzi mkuu baadaye mwezi huu. Razak amewaambia waandishi wa habari kwamba ana imani muungano anaouongoza wa National Front ambao umekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 55, utaibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo. Hata hivyo, weledi wa siasa za Malaysia wanaamini kuwa, kiongozi huyo atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kiongozi wa upinzani, Anwar Ibrahim. Kiongozi huyo wa upinzani aliwahi kukabiliwa na mashtaka ya ulawiti mwaka 2011 ingawa baadaye korti ilimpata bila hatia na kumuachilia huru. Baadaye Ibrahim alidai kuwa serikali ilipanga njama ya kumtupia kesi ya ulawiti ili kumvunja kisiasa. Malaysia ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani na tuhuma kama hiyo inachukuliwa kwa uzito mkubwa. Itakumbukwa kuwa, Muungano wa Najib Razak ulipata pigo kubwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2008 ambapo upinzani ulishinda viti 75 kati ya 222 na hivyo kuunyima muungano huo nafasi ya kuwa na thuluthi 2 ya viti inayohitajika kupitisha muswada bila tabu yoyote.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO