Kesi ya rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak imeahirishwa leo baada ya jaji Mostafa Hassan Abdallah aliyetarajiwa kuendesha kesi hiyo kujiondoa. Jaji huyo aliyetangaza uamuzi wake huo wakati wa kuanza kwa kesi ya Mubarak leo, sasa ameipeleka kesi hiyo katika mahakama ya rufaa na akisema haoni kama angelipenda kuendelea nayo.
Kesi ya Mubarak aliye na umri wa miaka 84 ilikuwa isikilizwe tena leo baada ya kesi ya kukata rufaa ya kupinga hukumu ya kifungo cha maisha iliotolewa dhidi yake kukubalika. Mubarak anakabiliwa na makosa ya mauaji katika maandamano ya kutaka mageuzi nchini humo yaliofanyika mwaka wa 2011.
Watoto wawili wa kiume wa Mubarak Gamal na Alaa, pamoja na mkuu wa usalama wa zamani Habib al-Adly pia wanakabiliwa na makosa sawa na kiongozi huyo wa zamani. Kulingana na shirika la habari la Mena la Misri wafuasi wa Mubarak wamekusanyika nje ya mahakama hiyo huku wakibeba picha zake.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO