Korea Kaskazini imedai kuondolewa vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na mpango wake wa nyuklia pamoja na majaribio yake ya makombora. Pia nchi hiyo inataka ahadi kutoka kwa Marekani kutoshiriki kile imekitaja kuwa ni "kitendo cha vita vya nyuklia" na Korea Kusini, kama kweli Marekani inataka paweko mazungumzo. Masharti hayo mapya yamekuja wakati kukiwa na hofu kuhusiana na uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya majaribio ya makombora. Mazungumzo yanayozihusisha pande sita, yaani Korea Kaskazini na Kusini, Japan, Marekani, Urusi na China yalikwama mnamo mwaka wa 2009. Rais wa Korea Kusini Park Guen Hye ameialika Korea Kaskazini katika meza ya mazungumzo ili kupunguza mvutano ambao umeongezeka kuhusiana na wasiwasi kuwa serikali ya Kaskazini inapanga kufyatua kombora. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry wameitaka Korea Kaskazini kurudi katika meza ya mazungumzo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO