Rais Barack Obama wa Marekani ametangaza
kuwa, Washington ina mpango wa kuiuzia silaha nchi ya Somalia iliyoko katika
Pembe ya Afrika. Marekani imetangaza utayarifu wake wa kuiuzia silaha Somalia
ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha
azimio la kusimamisha kwa muda wa mwaka mmoja vikwazo vya silaha dhidi ya
Somalia. Lengo la kupasishwa azimio hilo ni kuandaa uwanja kwa ajili ya
kuisaidia serikali ya Somalia ili iweze kukabiliana na makundi ya wanamgambo
likiwemo kundi la ash Shabab. Pamoja na hayo yote, uamuzi wa Marekani wa kuwa
tayari kuiuzia silaha Somalia haupaswi kutazamwa kwa jicho zuri; kwani ni
muendelezo ule ule wa siasa za kujitanua na za kupenda vita za viongozi wa
Washington ambazo zimekuwa zikipewa kipaumbele katika siasa za nje na viongozi
wa Ikulu ya White House katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. Swali wanalopaswa
kujiuliza walimwengu ni kuwa, kama kweli viongozi wa Marekani wanapigania
masuala ya kibinaadamu na amani nchini Somalia, walikuweko wapi katika kipindi
cha muongo mmoja uliopita wakati wananchi Waislamu wa nchi hiyo walipokuwa
wakitaabika kwa ukame na njaa? Kwa nini waliipuuza Somalia wakati huo tena
katika kipindi ambacho ilikuwa katika hali mbaya ya ukame na njaa? Ukweli wa
mambo ni kuwa, baada ya operesheni ya kijeshi ya Marekani kushindwa vibaya mwaka
1993 huko Somalia, na wanajeshi wake kuuawa mjini Mogadishu, viongozi wa
Washington waliipuuza na kuipa mgongo nchi hiyo masikini. Weledi wa mambo
wanaamini kuwa, mpango wa hivi sasa wa Marekani wa kuiuzia silaha nchi
iliyoharibiwa na machafuko ya Somalia hautakuwa na msaada wowote kwa serikali na
wananchi wa nchi hiyo. Hatua ya Marekani ya kutuma na kuuza silaha Somalia,
itaandaa uwanja wa kudumishwa vita, ukame, umasikini na kuvurugika zaidi hali ya
mambo katika nchi hiyo. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, hatua hiyo
ya Marekani inafanyika katika mfemu ya kushindana kisiasa na kijeshi na
Ufaransa. Marekani kama zilivyo Ufaransa na Uingereza, baada ya kumalizika
kipindi cha ukoloni barani Afrika, inatapatapa huku na huko ili kuhakikisha
kwamba, inapata upenyo wa kuwa na satua tena katika bara hilo lenye utajiri
mkubwa wa maliasili. Wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, mwezi Januari mwaka
huu, wakati Marekani ilipoitambua rasmi na kwa mara ya kwanza serikali ya
Somalia, walimwengu walipaswa kukihesabu kipindi hicho kuwa mwanzo wa kuanza
tena siasa za utwishaji mambo za Washington dhidi ya wananchi na serikali ya
nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO