Serikali ya Korea Kusini imetahadharisha kuwa, uwezekano wa kuzuka vita vya
nyuklia katika Peninsula ya Korea bado upo na hali ya mambo katika eneo hilo
imeendelea kuwa mbaya. Hii ni baada ya Korea Kaskazini kuwataka raia wa kigeni
kuondoka katika nchi jirani ya Korea Kusini ili wasije wakajipata katika
mazingira ya kutatanisha pindi vita vitakapoanza. Televisheni ya Taifa ya Korea
Kaskazini imesema makampuni ya kigeni mjini Seoul yanafaa kufungwa na kuwataka
watalii katika mji huo na kwingineko kuondoke mara moja. Huku hayo yakijiri,
mpaka wa China na Korea Kaskazini umefungwa kufuatia wasiwasi wa kutokea vita
katika Peninsula ya Korea. Hata hivyo kamanda wa ngazi za juu wa Marekani
amesema jeshi la nchi yake lina uwezo wa kuzuia makombora yote ya Korea
Kaskazini hata yale ya nyuklia. Pyongyang inazituhumu Marekani na Korea Kusini
kuwa zinakiuka haki yake ya kujitawala na imetishia kuzishambulia nchi hizo kwa
makombora ya nyuklia.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO