Wednesday, June 05, 2013

TANZANIA YAOMBA WALIMU WA HESABU NA SAYANSI TOKA JAPAN

Serikali ya Tanzania,  imeiomba Japan iisaidie walimu wa hisabati na sayansi na namna ya kufundisha walimu wa masomo hayo kama njia ya kukabiliana haraka na uhaba mkubwa wa walimu wa masomo hayo nchini humo. Tanzania ilitoa ombi hilo kwa Japan hapo jana, wakati rais wa nchi hiyo, Jakaya Mrisho Kikwete alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shirika la Ushirikiano na Misaada ya Kimataifa la Japan (JICA) Dakta Akihiko Tanaka mjini Yokohama. Tanzania imeiomba pia Japan kusaidia katika uchapishaji wa vitabu vya sayansi na hisabati ili kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi wa Tanzania anakuwa na nakala ya vitabu vya masomo hayo kama njia ya kuongeza ubora wa elimu nchini. Rais Kikwete alikuwa Japan kwa ziara ya siku saba kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika TICAD ambao umemalizika leo. Kikwete amesema kuwa, moja ya changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya elimu nchini Tanzania, ni ukosefu wa walimu wa hisabati na sayansi, masomo ambayo ni msingi muhimu wa maendeleo ya nchi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO