Wednesday, April 03, 2013

MULLAH OMAR RUKSA KUGOMBEA URAIS AFGHANISTAN


Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amesema kuwa kiongozi wa kundi la Taliban Mullah Mohammad Omar anaweza kugombea katika uchaguzi ujao wa rais uliopangwa kufanyika nchini humo mwezi Aprili mwakani. Rais Karzai amesema kuwa kiongozi huyo wa kundi la Taliban anaweza kuwa mgombea wa kiti cha urais na kuwapa fursa raia wa Kiafghani ya kumpigia kura ya ndio au hapana. Rais wa Afghanistan amesema kuwa katiba ya Afghanistan ni yenye uhalali kwa raia wote wa nchi hiyo na kwamba kundi la Taliban pia linapasa kunufaika na katiba hiyo. Rais Hamid Karzai ameyasema hayo siku chache baada ya kurejea kutoka safari ya kiserikali ya siku mbili huko Qatar ambako alijadiliana na viongozi wa nchi hiyo kuhusu uwezekano wa kufungua ofisi ya Taliban nchini humo kwa ajili ya mazungumzo ya kusaka amani. Mullah Omar amekuwa mafichoni tangu Marekani iishambulie kijeshi Afghanistan mwaka 2001. Hii ni katika hali ambayo mwezi Januari mwaka jana vyombvo vya habari vya Pakistan viliripoti kuwa polisi ya upelelezi ya Marekani FBI imeliondoa jina la kiongozi huyo wa Taliban katika orodha ya magaidi wanaosakwa kwa udi na uvumba na nchi hiyo. Washington ililiondoa jina la Mullah Omar katika orodha hiyo licha ya kulituhumu kundi la Taliban na kiongozi wa zamani wa Al Qaeda Osama bin Laden kuwa ndio waliohusika na mashambulio ya Septemba 11 nchini Marekani.  

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO