Sunday, April 21, 2013

TETESI KUHUSU UCHAGUZI WA RAIS IRAN

WAGOMBEA KITI CHA URAIS IRAN

Huku uchaguzi wa rais ukikaribia nchini Iran, joto la kisiasa linaendelea kupanda baada ya kuwepo tetesi kuhusu uwezekano wa kugombea tena marais wa zamani Akbar Hashemi Rafsanjani na Seyyed Mohammad Khatami.
Kwa mujibu wa Press TV, Mohammad Reza Aref ambaye alikuwa makamu wa kwanza wa rais Khatami amesema atajiondoa iwapo rais huyo wa zamani atagombea urais katika uchaguzi wa mwezi Juni. Hata hivyo mgombea Mohsen Rezaei amesema hatajiondoa hata kama marais wa zamani Rafsanjani na Khatami watagombea. Kwa mujibu wa sheria ya Iran, rais wa zamani anaweza kugombea urais baada ya kupita miaka mitano ya kumalizika muhula wake. Wakati huo huo mbunge mwandamizi Alireza Zakani naye amejitosa katika kinyang'anyiro cha urais nchini. Zakani ambaye ni katibu mkuu wa Jumuiya ya Wafuasi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza uamuzi wake Jumamosi usiku. Aidha waziri wa zamani wa afya Kamran Bagheri Lankarani ametangaza kugombea urais kwa tikiti ya Mrengo wa Waibua Hamasa ya Mapinduzi ya Kiislamu. Wengine waliotangaza nia ya kuwania urais wa Iran ni pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Mostafa Pour-Mohammadi, mwanachama mwandamizi wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo, Hassan Rohani na waziri wa zamani wa mambo ya nje Manoucher Mottaki. Rais Mahmoud Ahmadinejad anamaliza muhula wake wa pili na hivyo kikatiba hawezi kugombea. Uchaguzi wa rais Iran utafanyika Juni 14 na wagombea watajiandikisha kati ya Mei 7 na 11.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO