Walid al A’awadh Mjumbe wa Kamati ya Kisiasa ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) ametahadharisha juu ya njama za Wazayuni za kutayarishwa sehemu ya jangwa la Sinai la Misri kwa ajili ya makazi ya Wapalestina na kutangaza kuwa, eneo hilo kamwe halitokuwa nchi mbadala ya Wapalestina. Al A’awadhi amesema, watakabiliana vikali na kila mpango wa kuifanya nchi nyingine isiyokuwa ardhi yao asili ya Palestina kuwa nchi mbadala. Mjumbe huyo wa Kamati ya Kisiasa ya PLO ameongeza kuwa, kwa kisingizio cha kuwaounga mkono Wapalestina, wageni wanakusudia kuitenga sehemu ya Peninsula ya Sinai kama nchi yao mbadala, suala litakalozusha hitilafu nyingine kubwa kwenye eneo hilo. Sambamba na kusisitiza kuunga mkono ardhi yote ya Misri afisa huyo amesema, katika kipindi chote cha historia Wapalestina daima wamesimama kidete kukabiliana na njama za maadui, na kwamba hawatofumbia macho haki zao halali kisheria. Kitambo nyuma pia kulizungumziwa mpango wa kuundwa nchi ya Palestina huko Misri, suala lililokabiliwa na radiamali kali ya Wapalestina. Wakati huo Mussa Abu Marzuq miongoni mwa viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Wananchi wa Palestina (Hamas) ametangaza kupinga vikali Wapalestina mpango huo wa kuwahamishia katika jangwa la Sinai uliozungumziwa na duru za habari za Israel. Al Marzuq alipinga wazo la kuhamishiwa Wapalestina kwenye jangwa la Sinai na kusema kuwa, Wapalestina wanashikamana na ardhi zao na kwamba hawakubali eneo lolote badala yake. Sisitizo la Israel na waitifaki wake la kutekeleza mpango huo hatari wa kuwatafutia Wapalestina nchi mbadala linapignwa vikali na Wapalestina wenyewe na fikra za waliowengi duniani. Kuzungumziwa tena mpango wa nchi mbadala kwa ajili ya Wapalestina, kunadhihirisha kushtadi hatua za utawala huo na waitifaki wake za kuzuia kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baitul Muqaddas. Israel kwa njia tofauti inakusudia kupora kikamilifu haki za Wapalestina na katika kutimiza hilo inataka kuwakosesha wananchi wa Palestina hata haki ya kuishi kwenye nchi yao. Kwa msingi huo, inatumia kila njia kuzuia uwezekano wa kuundwa nchi ya Palestina katika ardhi ya Palestina. Israel inataka kufanikisha hilo kwa kujenga kwa wingi vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kutenganisha maeneo ya Palestina na maeneo mengineyo kwa uzio wa kibaguzi. Pia sambamba na kuzungumzia suala hilo, utawala huo ghasibu unakusudia kuandaa mazingira ya kuwafukuza kabisa Wapalestina nchini kwao na kujaribu kupotosha kadhia ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina kwenye nchi yao ili iweze kudhibiti kwa ukamilifu ardhi yote ya Palestina. Vilevile Israel inafuatilia mpango huo hatari wa nchi mbadala kwa ajili ya Wapalestina ili kufanikisha malengo yake ya kupenda kujitanua katika nchi za Kiarabu kama vile Misri. Kwa kuzusha wasiwasi miongoni mwa mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati, utawala wa Kizayuni unataka kufaidika na hali hiyo na kupotosha fikra za waliowengi juu ya kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Kwa ujumla utawala wa Kizayuni kwa njia tofauti unataka kuwazuia Wapalestina na jamii ya kimataifa kufuatilia suala la kutekelezwa maazimio ya Umoja wa Mataifa, na pia Wapalestina kupata haki zao kisheria kukiwemo kuundwa nchi huru ya Palestina. Inasemekana kuwa, mengi kati ya maazimio yaliyopitishwa katika Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Palestina yanasisitiza kuondoka Israel kwenye ardhi za Palestina na Wapalestina kupewa haki yao ya kuunda nchi huru mji mkuu wao ukiwa Baitul Muqaddas.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO