Carlos the Jackal ambaye alikuwa amejitwika uwanamapinduzi na wakati fulani alikuwa mmojawapo wa magaidi wanaosakwa kwa udi na uvumba duniani amefikishwa tena mahakamani nchini Ufaransa kukata rufaa ya kupinga hukumu ya kifungo cha maisha kwa kuhusika na mashambulizi kadhaa ya mabomu katika miaka ya 1980.
Wakati wa kuanza kwa kesi hiyo leo hii amewatimuwa mawakili wake na kuiomba mahakama imtafutie wengine.Raia huyo wa Venezuela mwenye umri wa miaka 63 ambaye jina lake halisi ni Ilich Ramirez Sanchez alihukumiwa kwa mara ya pili hukumu ya kifungo cha maisha hapo mwaka 2011 kwa kuhusika na mashambulizi ya mabomu hapo mwaka 1982 na mwaka 1983 ambayo yameuwa watu 11 na kujeruhi wengine zaidi ya 100. Amekanusha kuhusika kwa njia yoyote ile katika mashambulizi hayo.Kwanza alipatikana na hatia ya kuwauwa makachero wawili wa polisi wa Ufaransa na shushu mmoja wa Lebanon hapo mwaka 1975.
The Jackal kama alivyopachikwa jina hilo katika kitabu cha mwandishi riwaya Frederick Forsyth alikuwa ni mtu anayesakwa mno duniani wakati wa Vita Baridi wakati alipokuwa akipanga mashambulizi yaliohanikiza dunia dhidi ya mataifa ya magharibi.Carlos alikamatwa nchini Sudan na vikosi maalum vya Ufaransa hapo mwaka 1994 na tokea wakati huo yuko gerezani nchini Ufaransa.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO