Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al Maliki amesema kuwa, chama cha Baathi kilichong'olewa madarakani, ndicho kinachopanga mashambulizi ya kigaidi nchini humo. Al Maliki ameyasema hayo leo katika kikao na waandishi wa habari mjini Baghdad, Iraq. Akiashiria kuendelea kwa mashambulizi na miripuko nchini Iraq amesema, chama hicho cha Baathi kilichokuwa kikiongozwa na Saddam ndicho kinachopanga mashambulizi hayo na kwamba, hatua hiyo inaonyesha kuwepo kwa chuki za kikaumu nchini. Amesisitiza kuwa, viongozi wa chama hicho waliokuwa wakiwafukia watu wakiwa hai ndani ya kaburi moja, leo hii wafuasi wao wanaratibu na kutekeleza mashambulio ya mabomu katika maeneo ya watu wengi kama vile masokoni, misikitini na barabarani na kuwaua raia wengi wasio na hatia. Aidha waziri mkuu huyo wa Iraq amekosoa hatua ya baadhi ya vyama vya siasa kuunga mkono chama cha Baathi kilichofutwa nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, mapema leo watu 16 wameuawa na wengine 34 kujeruhiwa katika miripuko ya mabomu, iliyotokea katika maeneo mawili ya Sadr na Kamaliya katika viunga vya mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Aidha jana watu wengine 35 waliuawa na wengine 134 kujeruhiwa katika miripuko ya mabomu iliyotokea katika maeneo tofauti nchini humo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO