Waokoaji wamepata miili zaidi ndani ya vifusi vya jengo la kiwanda cha nguo lililoporomoka nchini Bangladesh, wakati maafisa wakisema huenda ikachukua siku nyingine tano kuondoa vifusi hivyo. Mbali na watu 430 waliothibitishwa kufa, polisi wameripoti kuwa wengine 149 bado hawajulikani waliko, kufuatia mkasa huo ambao ndio mbaya zaidi kuwahi kuikumba sekta ya nguo nchini Bangladesh. Miili 20 imegunduliwa usiku wa kuamkia leo huku waokoaji wakiamini kuwa miili zaidi imefunikwa katika ghorofa ya chini ya jengo hilo lililokuwa la ghorofa nane na sasa wanatumia mashine ili kuondoa vifusi hivyo. Wakati huo huo Meya wa mji wa Savar ambao mkasa huo ulitokea, Mohammed Refat Ullah, amewachishwa kazi kwa kuidhinisha kujengwa jumba hilo la Rana Plaza bila kufuata sheria. Mmiliki wa jengo hilo pamoja na babake ni miongoni mwa watu wanane wanaozuiliwa na polisi.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO