Marais Vladimir Putin wa Russia na Jacob Zuma wa Afrika Kusini walikutana na kufanya mazungumzo hapo siku ya Alkhamisi katika mji wa Sochi ulioko katika pwani ya Bahari Nyeusi nchini Russia. Hii ni mara ya tatu kwa Rais Zuma kufanya safari nchini Russia. Lengo la safari yake ya mara hii limetajwa kuwa ni kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili. Katika safari aliyofanya Rais Putin nchini Afrika Kusini mwezi Machi uliopita kwa lengo la kushiriki katika kikao cha tano cha Jumuiya ya Nchi Zinazoinukia Kiuchumi BRICS, nchi mbili hizo zilitiliana saini mikataba minane katika nyanja za nishati, utalii, usalama na ulinzi. Kwa msingi huo wataalamu wa mambo wanasema kuwa mazungumzo ya hivi sasa ya marais hao yamelenga kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili kwa msingi wa mikataba hiyo. Jumuiya ya BRICS ilipewa jina hilo miaka mitatu iliyopita baada ya Afrika kusini kujiunga na nchi za Brazil, Russia, India na China ili kufuatilia malengo ya kiuchumi. Rais Jacob Zuma anaamini kwamba Afrika Kusini ni mwakilishi wa nchi za bara la Afrika katika jumuiya hiyo na kwa hivyo anafanya juhudi za kuimarisha nafasi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya nchi hizo katika upeo wa kimataifa. Kwa kuwa na nguvu kubwa zaidi ya kiuchumi na kisiasa barani Afrika, Afrika Kusini inahesabiwa kuwa mshirika muhimu wa kibiashara wa Russia. Ni kutokana na ukweli huo ndipo uhusiano wa nchi hizo ukaimarika sana katika miaka ya hivi karibuni. Kwa kuimarisha uhusiano wa nchi yake na Russia ambayo ina nafasi muhimu katika ngazi za kimataifa, ni wazi kuwa Rais Jacob Zuma anataka kuinua zaidi nafasi ya kisiasa na kiuchumi ya Afrika Kusini katika upeo wa kimataifa. Mbali na masuala ya pande mbili na vilevile udharura wa kuasisiwa benki ya ustawi ya BRICS, Marais Putin na Zuma pia wamejadili suala la kufanyiwa marekebisho mfumo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kama ilivyo Russia, Afrika Kusini inataka baraza hilo lifanyiwe marekebisho ya kiidara na kimuundo. Afrika Kusini, Nigeria na Algeria ni nchi za bara la Afrika ambazo zinajadiliwa kupewa uanachama wa kudumu katika baraza hilo. Migogoro ya Mali, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mambo mengine yaliyojadiliwa na viongozi wa nchi mbili hizo. Safari ya Jacob Zuma nchini Russia pia imekuwa na malengo ya kisiasa na kipropaganda ikitiliwa maanani kwamba rais huyo ambaye ni mgombea wa chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini anajiandaa kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini mwezi Aprili mwaka ujao. Kwa kuimarisha uhusiano wa kimataifa wa nchi yake, Rais Zuma anatarajia kuwa jambo hilo litamurahisishia njia ya kuhudumia tena nafasi hiyo baada ya kufanyika uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO