Waasi huko Sudan Kusini wameteka kituo cha kijeshi na mji wa Boma katika jimbo la Jonglei baada ya mapambano makali na jeshi mashariki mwa nchi hiyo.
Waasi hao wanaoongozwa na David Yau Yau wajulikanao kama South Sudan Democratic Army (SSDA) wanasema wanataka kumaliza ufisadi na mfumo wa chama kimoja wa serikali ya SPLM.
Mwezi Machi jeshi la Sudan Kusini lilianzisha oparesheni dhidi ya kundi hilo la Yau Yau katika jimbo la mashariki la Jonglei. Sudan Kusini inataka kuanza kufanya oparesheni za kuchimba mafuta katika eneo hilo kwa msaada wa shirika la Ufaransa la Total. Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya watu wameachwa bila makao katika mapigano ya hivi karibuni.
Msemaji wa SSDA Peter Konyi Kubrin amesema waasi wamepata miili ya wanajeshi 50 wa serikali baada ya kuchukua udhibiti wa mji wa Boma. Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer amesema wanajeshi wameondoka katika kituo chao mjini Boma na kuelekea juu ya mlima ujulikanao kama Upper Boma. Amesema wanapanga kuwatimua waasi hao. Tokea Sudan Kusini ijitenge na Sudan mwaka 2011 imeshindwa kukabiliana na waasi katika nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO