Katika kuendeleza mashauriano ya kidiplomasia katika eneo la Mashariki ya Kati, Ali Akbar Salehi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran baada ya kuitembelea Jordan alielekea mjini Damascus ambako alikutana na Rais Bashar al Assad wa Syria na kujadili mabadiliko ya kieneo na mgogoro wa nchi hiyo. Katika mazungumzo yake hayo ya masaa machache na Assad siku ya Jumanne mjini Damascus, Salehi alielezea jitihada za Jamhuri ya Kiislamu katika eneo na kimataifa kwa ajili ya kurejesha amani, usalama na utulivu wa Syria. Pia alisema kwamba, njia pekee ya kutatuliwa mgogoro wa Syria ni mazungumzo ya kisiasa ya pande za Syria bila uingiliaji wa askari wa kigeni nchini humo. Rais Bashar la Assad pia alisisitiza azma ya serikali na wananchi wa Syria ya kukabiliana na kila njama za ndani na nje dhidi ya nchi yao. Safari ya masaa machache ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mjini Damascus na pia mazungumzo yake na viongozi wa Jordan, yana umuhimu mkubwa. Kwanza kwa kuzingatia kuwa Iran ni mwenyekiti wa Jumuiya Isiyofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM, mazungumzo hayo yanaambatana na mtazamo mpana juu ya masuala ya amani na usalama wa eneo hili. Pili ni kwa kuwa, ili kusaidia kutatua mgogoro wa Syria, Iran inasisitiza zaidi kuhitimishwa haraka machafuko na kuanza mazungumzo kuliko hatua nyingine zozote. Hii ni kwa sababu, uingiliaji wowote wa kijeshi au kuchochea mgogoro wa nchi hiyo kunaweza kuhatarisha zaidi usalama wa eneo zima. Kwa ajili hiyo, Iran inapinga njia za kutumiwa nguvu na mashambulio dhidi ya nchi yoyote huru, na inaamini kuwa wale wanaotaka kutumiwa njia hizo, bila shaka wanafuatilia malengo yao haramu katika eneo hili.
Mgogoro wa Syria umeshtadi na kupanuka kutokana na uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa makundi ya kigaidi ya nchi hiyo. Kutokana na uungaji mkono huo ambapo hivi karibuni makundi ya kigaidi ya Syria yalianza kusaidiwa silaha nzito, eneo la Mashariki ya Kati linakabiliwa na hatari ya kukosa amani na usalama. Hivi sasa kuna pande mbili zinazojulikana nchini Syria. Upande mmoja ni ule unaotaka kufanya mazungumzo na serikali na unoafadhilisha suluhisho la kisiasa kuliko mapigano. Upande wa pili ni makundi yanayopenda vita na machafuko kama Harakati ya al Nusra iliyoungana na kundi la al Qaida, huku malengo yao yakiwa wazi kabisa. Kutokana na uungaji mkono wa baadhi ya nchi kwa makundi ya kigaidi ya Syria, katika miezi kadhaa iliyopita vitendo vya kigaidi vya makundi hayo vimeongezeka, na kuanza kuzusha hitilafu kati ya Waislamu hasa wa madhehebu ya Sunni na Shia. Kwa ajili hiyo tunaweza kusema kuwa, mwenendo wa kuingilia masuala ya ndani ya Syria hautabiriki, na katika kufanikisha mweneno huo, Marekani na Israel kwa kushirikiana na nchi khadhaa za Kiarabu na Uturuki zimeanza harakati mpya dhidi ya Damascus ikiwa ni pamoja na kupangwa na kutekelezwa shambulio la anga la lililotekelezwa hivi karibuni na Israel dhidi ya Syria. Baada ya kuonana na Assad ingawa Salehi alisema kwamba, kusimama kidete wananchi na kushirikiana na serikali, kumesababisha mfumo wa kisiasa wa Syria uweze kuhimili mashinikizo ya nje na mamluki wenye silaha wa ndani, lakini amezitahadharisha nchi za eneo hili juu ya matokeo ya kuwepo ombwe ya kisiasa nchini Syria.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO