Shirika kubwa la ndege la Ujerumani Lufthansa na chama cha wafanyakazi cha verdi vimekubaliana nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi takriban 33,000 wa shirika hilo.Shirika la habari la Ujerumani dpa limesema leo kuwa wafanyakazi hao watapata nyongeza ya kati ya asilimia 3 na 4.7 na kuhakikishiwa kazi zao kwa kipindi cha miezi 26 ijayo.Wiki iliyopita wafanyakazi hao wa Lufthansa walishiriki katika mgomo wakidai nyongeza ya mishahara.Karibu ndege 1700 zilisitisha usafiri kutokana na mgomo huo ambao uliwawacha zaidi ya abiria 150,000 wakiwa wamekwama.Mwanzoni chama hicho cha wafanyakazi kilitaka nyongeza ya asilimia 5.2 na hakikisho la kusalia katika ajira kwa miezi 29. Lufthansa inajaribu kupunguza gharama ili kukabliana na bei ya juu ya mafuta na ushindani mkali kutoka mashirika mengine ya ndege ya Ulaya na kutoka eneo la ghuba kama Emirates,Qatar na Etihad.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO