Kusambazwa hivi karibuni picha zilizoonyesha kuuawa kinyama kwa askari mmoja wa Uingereza katika moja ya mitaa ya London kumeongeza wasiwasi wa Waislamu wa nchi hiyo walio na hofu ya kuongezeka vitendo vya dhulma na ukandamizaji dhidi yao. Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza imetoa taarifa ikikosoa kuenezwa propaganda dhidi ya Uislamu kufuatia mauaji hayo na kutaka kusimamishwa mara moja kwa uchochezi wa chuki unaofanywa dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Kamisheni hiyo imesisitiza kwamba polisi ya nchi hiyo inapasa kuchukua hatua za dharura za kulinda usalama wa Waislamu pamoja na kukabiliana na makundi ya ubaguzi wa rangi yanayotaka kutumia vibaya tukio hilo dhidi ya Waislamu. Kamisheni hiyo pia imeitaka polisi ya London kuimarisha usalama katika misikiti, shule na vituo vya Kiislamu mjini humo. Kuakisiwa kwa kiwango kikubwa kwa mauaji ya askari huyo wa Uingereza na vyombo vya habari vya nchi hiyo na wakati huohuo kuhusishwa mauaji hayo na Waislamu kumepelekea baadhi ya makundi yenye fikra na mielekeo ya kupindukia mipaka kuwatisha Waislamu na kuonya kwamba yatalipiza kisasi dhidi yao. Askari huyo mwenye umri wa miaka 25 kwa jina la Lee Rigby aliuawa kwa kisu siku ya Jumatano katika mtaa wa Woolwich kusini mashariki mwa London. Mara tu baada ya kuawa askari huyo vyombo vya habari vya Uingereza viliwaarifisha wahusika wa tukio hilo kuwa ni vijana wawili wa Kiislamu na kisha kurusha hewani ripoti nyingi hasi dhidi ya Waislamu. Kuafutaia mauji hayo, David Cameron Waziri Mkuu wa Uingereza ambaye alikuwa safarini nchini Ufaransa alikatiza safari hiyo na kurejea Uingereza kwa lengo la kuongoza kikao cha dharura cha kuchunguza tukio hilo. Akizungumza baada ya kumalizika kikao hicho alisema kuwa lawama za mauaji hayo zinapaswa kuelekezwa kwa waliohusika tu bila ya kuihusisha dini yoyote. Cameron amesisitiza kwamba wananchi wote wa Uingereza bila kujali dini wala utamaduni wao wamekasirishwa na kulaani tukio hilo la kinyama na kuongeza kuwa tukio hilo si tu kwamba limeshambulia Uingereza na mfumo wa maisha wa raia wa nchi hiyo bali pia ni hiana ya wazi dhidi ya Uislamu na Waislamu wanaoishi nchini humo. Amesisitiza kwamba hakuna sehemu yoyote katika Uislamu ambapo kitendo kama hicho kinahalalishwa. Taasisi na mashirika tofauti ya Kiislamu nchini Uingereza likiwemo Baraza la Waislamu wa nchi hiyo yametoa taarifa tofauti yakilaani tukio hilo na kusisitiza kuwa Uislamu hauungi mkono kitendo kama hicho cha kishetani. Taasisi hizo zimetaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahalifu waliohusika na mauaji hayo kwa madai eti ya kuwatetea Waislamu. Wakati huohuo kundi moja la wabaguzi wa rangi linalodai kutetea maslahi ya Waingereza siku ya Jumatano lilikusanyika katika eneo la tukio hilo na kupiga nara za chuki na ubaguzi wa rangi dhidi ya Waislamu. Tunakumbusha hapa kuwa vitendo vya chuki na uadui vimeongezeka sana dhidi ya Waislamu wanaoishi katika nchi za Ulaya katika miaka ya hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO