Saturday, June 01, 2013

JAPAN KUTOA MSAADA WA DOLA BILIONI 32 KWA AFRIKA

Japan imeahidi kutoa msaada wa dola bilioni 32 kuzisaidia sekta za umma na za binafsi katika nchi za bara la Afrika ili kusaidia ustawi na maendeleo na kuyashajiisha mashirika na makampuni ya Kijapani kuwekeza barani humo katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Ahadi hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo wa Maendeleo ya Afrika (TICAD) na inajumuisha msaada rasmi wa maendeleo wa dola bilioni 14 na dola bilioni 6.5 za kusaidia sekta ya miundombinu. Kwa mujibu wa takwimu rasmi kiwango cha uwekezaji wa moja kwa moja wa Japan barani Afrika katika mwaka 2011 kilikuwa dola milioni 460 kikiwa ni cha chini mno kulinganisha na uwekezaji wa dola bilioni 3.17 uliofanywa na China katika nchi za bara hilo. Tangu achaguliwe kuwa Waziri Mkuu wa Japan mwezi Disemba mwaka uliopita, Shinzo Abe amechukua hatua kubwa katika uga wa diplomasia na amesisitiza kwamba anapanga kufanya safari katika nchi za Kiafrika mapema iwezekanavyo. Inafaa kuashiria kuwa viongozi wapatao 50 wa nchi za bara la Afrika wanashiriki katika mkutano wa siku tatu wa TICAD unaofanyika huko Yokohama karibu na mji mkuu wa Japan, Tokyo unaojadili masuala kadhaa yakiwemo ya maendeleo ya uchumi, kuleta amani na kupambana na uharamia

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO