Jeshi la Polisi nchini Ufaransa limelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za plastiki kuwatawanya watu waliopandwa na hasira, baada ya askari polisi kumkamata mwanamke aliyevaa burqa ya Kiislamu pambizoni mwa Paris, mji mkuu wa nchi hiyo. Duru za polisi zinaeleza kuwa, machafuko hayo yalianza jana usiku baada ya polisi kumsimamisha mwanamke huyo wa Kiislamu mwenye umri wa miaka 25 kwenye eneo hilo la kaskazini magharibi mwa Paris ambalo linakaliwa na idadi kubwa ya Waislamu. Duru hizo zimeeleza kuwa, kundi la vijana wasiopungua 60 lilijitokeza na kuzuia kutiwa nguvuni mwanamke huyo aliyevaa hijabu, jambo ambalo lilipelekea askari polisi kushambuliwa na Waislamu hao wenye hasira. Kwa mujibu wa sheria za Ufaransa, uvaaji wa burqa ulipigwa marufuku tokea mwanzoni mwa mwaka 2011, suala ambalo limekabiliwa na upinzani mkali wa Waislamu nchini humo. Kosa la uvaaji wa burqa ni kupigwa faini ya dola 190 au kupelekwa kwa nguvu kwenye mafunzo ya uraia.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO