Saturday, June 22, 2013

MAANDAMANO YAENDELEA UTURUKI

Maandamano ya Waturuki dhidi ya serikali bado yanaendelea na mara hii waandamanaji wameamua kudumisha maandamano hayo kwa kukaa kimya na kutotoa nara zozote. Maandamano hayo yaliyoanza tarehe 28 Mei yamepelekea watu watano kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Licha ya kuendelea maandamano lakini hakuna mabadiliko wala dalili zozote zinazoashiria kwamba serikali ya Ankara imelegeza msimamo mbele ya matakwa ya waandamanaji. Kufikia sasa polisi ya Uturuki imetumia zaidi ya mikebe laki moja na 30,000 ya vinyunyuzio vya pilipili dhidi ya waandamanaji, jambo ambalo si la kawaida. Suala hilo limepelekea Shirikisho la Kimataifa la Jumuiya za Haki za Binadamu kutaka kutouziwa Uturuki gesi ya kutoa machozi. Shirikisho hilo linasema kwamba kutumiwa vibaya gesi hiyo pamoja na risasi za plastiki ni jambo linalokwenda kinyume na sheria za kimataifa pamoja na misingi ya Umoja wa Mataifa. Inasemekana kuwa watu 10 wamefanywa kuwa vipofu na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na hatua ya polisi ya kutumia vibaya gesi na risasi hizo. Wakati huohuo serikali ya Ankara iko mbioni kupasisha sheria ambayo itaiwezesha kukabiliana vikali na watu ambao wataeneza kwenye vyombo vya habari masuala ambayo yataonekana kuwa ni kuchochea wananchi dhidi ya serikali. Jambo la kushangaza hapa ni kuona jinsi serikali ya Uturuki inafuatilia kwa karibu mbinu za kukandamiza maandamano na harakati za kiraia nchini humo, jambo ambalo linachukuliwa na wananchi kuwa lisilo la kidemokrasia. Maandamano hayo ambayo yamekuwa yakiendelea nchini humo kwa kipindi cha wiki tatu sasa yameathiri pakubwa sekta ya utalii ambayo ni tegemeo muhimu la pato la kigeni kwa nchi hiyo. Mandamano hayo pia yamepunguza sana thamani ya sarafu ya nchi hiyo na kuvuruga kabisa uwekezaji wa kigeni nchini. Iwapo ghasia zinazotokana na maandamano hayo zitaendelea, ni wazi kuwa zitaathiri pakubwa uchumi wa nchi hiyo inayotegemea utalii na uwekezaji wa kigeni. Tayari ghasia hizo zimeiletea nchi hiyo hasara ya lira trilioni 1.4. Licha ya hayo, hatua ya polisi ya kutumia nguvu za ziada dhidi ya waandamanaji ni jambo ambalo limezusha hitilafu miongozi mwa wanachama wa chama tawala cha Uadilifu na Ustawi na vilevile kati ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya. Waatalamu wa mambo wanasema kuwa kuendelea kwa mgogoro wa Uturuki kwa upande mmoja na kuendelea ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji kwa upande wa pili, kumevuruga kabisa mafanikio ya kiuchumi ya Recep Tayyip Erdoğan Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Uadilifu na Ustawi. Kwa vyovyote vile kuendelea ukandamizaji wa polisi ya Uturuki dhidi ya waandamanaji na hatua ya serikali ya Erdogan ya kutolegeza msimamo mbele ya mashinikizo ya waandamanaji, ni jambo linalobatilisha moja kwa moja madai ya serikali ya Ankara kwamba inaheshimu misingi ya demokrasia.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO