Marekani itatuma mitambo ya kuzuia makombora ya Patriot na ndege za kivita aina ya F16 nchini Jordan kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi, na imesema vifaa hivyo vinaweza kuendelea kuwepo nchini humo ili kukabiliana na tishio lolote linaloweza kutokana na mgogoro wa Syria. Msemaji wa kamandi kuu ya jeshi la Marekani iliyopo Tampa Bay Florida, Luteni Kanali T.G. Taylor, alisema zana hizo ziliidhinishwa kama sehemu ya mazoezi yaliyopewa jina la "Eager Lion" yenye lengo la kuimarisha uwezo wa kijeshi wa Jordan. Hata hivyo, maafisa wa Marekani wamekataa kusema ni ndege ngapi za kivita zitashiriki mazoezi hayo ya pamoja, au ngapi zitabakia nchini Jordan baada ya zoezi hilo. Marekani iliunga mkono hatua kama hiyo mapema mwaka huu nchini Uturuki, ambako jumuiya ya kujihami NATO imeweka mitambo ya Patriot katika mpaka wa nchi hiyo na Syria.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO