Mara baada ya kukaliwa kwa mabavu Afghanistan, raia kadhaa wa nchi hiyo walitiwa mbaroni na kupelekwa kwenye jela ya kuogofya ya Guantanamo kwa madai kuwa ni magaidi au wanayasaidia makundi ya kigaidi, kwa mujibu wa madai ya viongozi wa serikali ya Marekani. Mara kadhaa Rais Barack Obama wa Marekani alisikika wakati wa kampeni za urais mwaka 2008 akitoa ahadi kwamba katika kipindi cha siku 100 tu tokea atakapoingia madarakani atahakikisha anaifunga moja kwa moja jela ya Guantanamo, lakini ahadi hiyo imeota mbawa na hadi sasa bado hajaitekeleza na badala yake amekuwa akitoa visingizio kadhaa visivyo na mashiko. Hii ni katika hali ambayo, Bunge la Marekani limepiga kura kuhusiana na kuendelea shughuli za jela hiyo ya kuogofya. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kamati moja maalumu ya bunge la nchi hiyo, ilipiga kura ya kuendelea shughuli za jela hiyo kwa kipindi kisichojulikana. Hatua hiyo inathibitisha na kuipa meno sheria ya hivi sasa inayopiga marufuku utumiwaji wa fedha za walipa kodi wa nchi hiyo kwa minajili ya kujenga jela nyingine au kuwahamishia mahabusu wa Guantanamo ndani ya ardhi ya Marekani. Maamuzi ya kamati hiyo maalumu ya bunge yanakinzana wazi na matamshi yaliyotolewa na Rais Obama mwezi uliopita ya kuifunga jela ya Guantanamo. Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ‘Pentagon’ hivi karibuni ililiomba Baraza la Kongresi la nchi hiyo kupitisha bajeti ya dola milioni 450 kwa lengo la kuiboresha jela ya Guantanamo. Pentagon inadai kuwa, gharama za kila mwaka za kumtunza kila mfungwa kwenye gereza hilo ni sawa na dola laki tisa na kwamba suala hilo limesababisha Guantanamo kuhesabiwa moja kati ya jela zenye gharama za juu duniani. Hivi sasa kuna migongano kati ya matamshi ya Rais Obama ya kutaka kuifunga jela ya Guantanamo na Wizara ya Ulinzi ya Marekani inayosisitiza juu ya kupatiwa fungu zaidi la bajeti ya kuendeshea jela hiyo. Licha ya hayo, Pentagon imeomba dola milioni 200 kwa ajili ya kulijenga jeshi la Marekani kwa shabaha ya kuboresha taasisi zake za muda ambapo kuna uwezekano ujenzi huo ukachukua muda wa miaka minane hadi kumi, kwani jeshi linapaswa kuwapeleka wajenzi na vifaa vyao kwa njia ya anga huko Cuba. Hii ni katika hali ambayo, mahabusu 130 kati ya 166, wanaoshikiliwa kwenye jela ya Guantanamo wamefanya mgomo wa kula yapata miezi minne sasa. Mahabusu wameamua kufanya mgomo huo wa kula wakilalamikia hali mbaya ya jela hiyo, kushikiliwa kwa muda usiojulikana, kusailiwa mara kwa mara mambo yao binafsi kunakofanywa na askari magereza na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu. Serikali ya Marekani imewapa amri madaktari wa jela hiyo ya kuwalisha chakula kwa nguvu mahabusu hao kupitia njia ya kuwaweka mirija puani ili waendelee kubaki hai. Watu wengi wanaamini kwamba kitendo hicho ni dhihirisho la wazi la mateso wanayoyapata mahabusu hao. Hatua ya mahabusu wa Guantanamo ya kugoma kula chakula, imesababisha jamii ya kimataifa kuichukia mno serikali ya Marekani ambapo kwa mara nyingine tena Rais Obama ameonyesha kushindwa kutekeleza ahadi zake baada ya kupita miaka mitano tokea aingie madarakani. Inafaa kuashiria hapa kuwa, hali mbaya ya jela ya Guantanamo iliyopelekea serikali ya Marekani hapo kabla kuwahamishia baadhi ya mahabusu hao nchini Marekani na baadhi yao kuwaachilia huru, kutokana na mashinikizo makubwa yaliyotolewa na fikra za walio wengi duniani na hali kadhalika ripoti kadhaa za ukosoaji zilizotolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu za kuitaka Washington iifunge jela hiyo, lakini suala hilo lilikabiliwa na upinzani wa Baraza la Kongresi na hivi sasa hatima ya jela hiyo ya kuogofya haijulikani. Inaonekana kuwa, hatua ya kamati maalumu ya bunge la Marekani ya kuunga mkono mwendelezo wa shughuli za jela ya kuogofya ya Guantanamo, inaleta matumaini madogo mno ya kufungwa jela hiyo hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO