Mkuu wa kitengo cha usalama katika ofisi ya Rais wa Guinea Conakry ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki kwenye mauaji dhidi ya wananchi wa nchi hiyo. Jean Claude alifikishwa mahakamani hapo jana kujibu shitaka la kushiriki kwenye mauaji ya wananchi wa nchi hiyo Septemba 28 mwaka 2009. Afisa mwandamizi kutoka shirikisho la kimataifa la mashirika ya haki za binadamu ameelezea kufurahishwa kwake na hatua ya kumtia mbaroni na kumfungulia mashtaka Jean Claude. Amesema kuwa hatua hiyo inaonyesha jinsi Guinea ilivyopiga hatua kuleta haki na usawa nchini humo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, tarehe 28 Septemba 2009, maelfu ya wapinzani wa serikali ya Guinea walikusanyika katika uwanja mjini Conakry kupinga hatua ya Mousa Dadis Camara ambaye alikuwa Mkuu wa Baraza la Kijeshi linalotawala nchini humo kutaka kushiriki kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais mwaka 2010. Vikosi vya usalama vya nchi hiyo viliingia uwanjani hapo na kuwapiga, kuwafyatulia risasi na hata kuwabaka wanawake waliokuwepo uwanjani hapo. Machafuko hayo yalisababisha watu wasiopungua 157 kuuawa na wanawake zaidi ya 100 kubakwa na vikosi vya usalama vya nchini humo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO