Ujumbe wa kidiplomasia unaoongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia ambaye pia ni mkuu wa Kituo cha Amani cha nchi hiyo umewasili mjini Cairo Misri kwa ziara ya siku tatu kwa lengo la kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo.
Baada ya Ethiopia kuchukua uamuzi wa kujenga bwawa la Renaissance au ambalo mara nyingine linajulikana kwa jila la Millennium Dam, kwenye Mto Nile na hivyo kuzusha mvutano katika uhusiano wa nchi hizo, hii ni mara ya kwanza kwa ujumbe wa kidiplomasia wa Ethiopia kufanya safari nchini Misri. Kamati ya Wataalamu wa Kimataifa inasema kuwa uamuzi wa Ethiopia wa kujenga bwawa hilo katika mto uliotajwa unahatarisha maslahi ya nchi mbili za Misri na Sudan zinazonufaika kwa sehemu kubwa na maji ya mto huo. Kamati hiyo ambayo inajumuisha wataalamu kutoka nchi za Ethiopia, Sudan, Misri, Afrika Kusini, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, ilibuniwa sambamba na kuanza shughuli za ujenzi wa bwala la Renaissance ili kutathmini manufaa ya nchi tatu za Ethiopia, Misri na Sudan kutokana na maji ya Mto Nile. Kamati hiyo imetayarisha ripoti ya kurasa 800 na kuiwasilisha kwa serikali za nchi hizo tatu ili zipate kuifanyia kazi. Mwishoni mwa mwezi Mei uliopita serikali ya Ethiopia ilianza kubadilisha mkondo wa maji ya Mto Blue Nile ambao unachangia sehemu kubwa ya maji ya Mto Nile na kuyaelekeza kwenye mradi wa bwawa hilo ambalo linatathminiwa kugharimu dola bilioni 4 na milioni 700. Mto wa Blue Nile huungana na wa White Nile katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na kuunda Mto Nile na kupitia ardhi ya Misri kabla ya kumwaga maji yake kwenye bahari ya Mediterranean. Kwa msingi huo, kujengwa bwawa la Renaissance kwenye mto huo kumeitia wasiwasi mkubwa Misri ambayo inahofia kwamba huenda ikapoteza hisa kubwa ya maji ya mto huo. Licha ya makelele mengi yaliyopigwa na Misri kuhusiana na suala hilo lakini mazungumzo ya hivi karibuni ya ujumbe wa kidiplomasia wa nchi hiyo huko mjini Addis Ababa Ethiopia, yalikuwa na mafanikio. Licha ya upinzani wa Misri wa kujengwa bwawa hilo kwenye Mto Nile lakini Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameunga mkono mradi huo muhimu wa Ethiopia na kusema kuwa umeme utakaozalishwa na bwawa hilo utazifaidi nchi nyingi zinazopakana au kuchangia maji ya Mto huo.
Katika upande wa pili Ban Ki-moo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka nchi mbili za Misri na Ethiopia kutatua kwa amani hitilafu zao kuhusiana na suala hilo. Amemtaka Rais Muhammad Mursi wa Misri ambaye ametishia kuingia kwenye vita ili kutetea maslahi ya nchi yake kuhusiana na maji ya Mto Nile kuketi pamoja na Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn wa Ethiopia kwenye meza ya mazungumzo ili kutatua kwa njia za kidiplomasia matatizo yaliyopo. Wakati huohuo hivi karibuni bunge la Ethiopia lilipasisha mswada mpya ambao utachukua nafasi ya mkataba wa kikoloni ambao inazipa nchi za Sudan na Misri fursa ya kunufaika na maji ya Mto Nile. Mkataba huo pia ulitiwa saini na nchi sita zinazopakana na mto huo. Kwa mujibu wa mswada huo, nchi zote zinazochangia maji ya mto huo sasa zinaruhusiwa kunufaika na maji hayo katika kuanzisha miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO