Thursday, July 11, 2013

BINTI WA KISAUDIA ASHTAKIWA MAREKANI KWA KUMTESA MTUMISHI

Binti Mfalme Msaudi ameshtakiwa Marekani kwa usafirishaji haramu wa binaadmau na kumlazimu mwanamke Mkenya kumfanyia kazi nyumbani kwake. Bi. Meshael Alayban mwenye umri wa miaka 42 ambaye alitambuliwa kama binti mfalme wa Saudi Arabia amefikishwa mahakamani Jumatano katika Jimbo la California nchini Marekani kwa tuhuma za kumuweka kinyume cha sheria mwanamke raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 30. Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Orange County Tony Rackauckas, Alayban anakabiliwa na shtaka la kusafirisha mwanaadamu kinyume cha sheria na akipatikana na hatia atafungwa kifungo cha miaka 12 gerezani. Mkenya huyo ambaye jina lake halikutajwa anasema alipata kazi hiyo mwaka 2012 akiwa Kenya lakini alipowasili Saudi Arabia pasipoti yake ilichukuliwa. Anasema amekuwa akilazimishwa kufanya kazi kwa muda mrefu pasina kupumzika na kwa malipo duni. Aidha amekuwa akifanya kazi bila ya mkataba. Binti mfalme huyo wa Saudia ameachiliwa huru kwa dhamana ya dola milioni tano na hawezi kuondoka Marekani bila idhini. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la wanawake Wakenya wanaoteswa vibaya na waajiri wao nchini Saudi Arabia na hata baadhi wamepoteza maisha kutokana na mateso waliyopata.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO