Thursday, July 04, 2013

IRAN YAWAKUMBUKA RAIA WALIOUAWA KWA KUSHAMBULIWA NDEGE YAO NA JESHI LA MAREKANI

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeadhimisha mwaka wa 25 tangu kuuawa shahidi abiria wa ndege ya Shirika la Ndege la Iran Air ambayo ilitunguliwa kwa makombora ya manowari ya kivita ya Marekani.
Katika hujuma hiyo ya kigaidi ndege ya abiria aina ya Airbus ya Shirika la Ndege la Iran Air iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas, kusini mwa Iran, na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo wakiwemo wanawake na watoto wachanga. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama wa serikali ya Marekani.
Kumbukumbu ya tukio hilo imefanyika leo kusini mwa Iran katika Ghuba ya Uajemi na kuhudhuriwa na maafisa wa kijeshi katika balozi kadhaa za kigeni nchini Iran. Katika ujumbe wake kwa hafla hiyo Mkuu wa Vikosi vyote vya majeshi ya Iran Meja Jenerali Sayyid Hassan Firuzabadi ametaka hatua zichukuliwe ili kuzuia kukaririwa tena jinai kama hiyo ya Marekani.
Naye Brigedia Jenerali Farzad Esmaili kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Iran amesema tukio la kutunguliwa ndege ya abiria ya Iran ni dalili ya wazi kuwa Marekani inawahadaa walimwengu inapodai kutetea haki za binaadamu. Kwa upande wake Jenerali Rahim Mumtaz mwambata wa kijeshi wa Ubalozi wa Pakistan nchini Iran ambaye alizungumza kwa niaba ya wambata wa kijeshi katika hafla hiyo amesema tukio la kutunguliwa ndege hiyo ya Iran ni jinai kubwa ambayo inapaswa kulaaniwa na watu wote.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO