Thursday, July 04, 2013

M23 WATISHIA KUUTEKA TENA MJI WA KIVU

Kundi la waasi wa M23 la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetishia kulitwaa tena jimbo la Kivu kaskazini lililoko mashariki mwa nchi hiyo.
Waasi wa M23 wametishia kwamba watauteka tena mji wa Goma makao makuu ya jimbo hilo, iwapo mazungumzo kati ya kundi hilo na serikali ya Kinshasa yatavunjika. Afisa mmoja wa kundi la waasi wa M23 amefichua kwamba, mji wa Goma utatekwa tena, kwa sababu serikali ya Kinshasa haitaki kutekeleza matakwa yao.
Kiongozi huyo amesema kuwa, serikali ya Kongo badala ya kukidhi matakwa ya waasi inakitegemea zaidi kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa cha kukabiliana na makundi yenye silaha mashariki mwa nchi hiyo kwa dhana kwamba kinaweza kutatua matatizo ya Kongo. Amesema kuwa, tokea kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kinachoundwa na nchi za Tanzania, Afrika Kusini na Malawi kiingie nchini Kongo, serikali ya Kinshasa imekuwa ikifanya jitihada za kuwalazimisha waasi wapokonywe silaha na kutia saini makubaliano ya amani bila ya kufanyika mazungumzo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO