Jeshi nchini Marekani limeweka hadharani gharama, hatari na faida ambazo zinaweza zikapatikana iwapo nchi hiyo itafanya uvamizi wa kijeshi nchini Syria kwa lengo la kuiangusha Serikali ya Rais Bashar Al Assad inayopambana na Waasi kwa kipindi cha miezi ishirini na nane sasa. Kiongozi wa Juu kwenye Jeshi nchini Marekani Jenerali Martin Dempsey amekiri kuna hatari kubwa na gharama kubwa iwapo nchi hiyo itaivamia kijeshi nchini Syria kitu ambacho kinaweza kikaleta madhara makubwa kwa mustakabali mwema wa baadaye wa nchi hiyo. Jenerali Dempsey ametoa mapendekeo matano ya kijeshi katika kushughulikia mgogoro huo wa Syria akithibitsha udhibiti wa mashambulizi pamoja na kuanzishwa kwa sheria za kuzuia matumizi ya anga la taifa hilo.
Kiongozi huyo wa Kijeshi ameliambia Bunge nchini Marekani kwamba kitendo cha kutumia kikosi cha kijeshi kinaweza kikawa kama vita na huenda vikaleta hasara kubwa kwa taifa hilo na kulazimika kutumia mabilioni ya walipa kodi. Miongoni mwa mambo mengine ambayo amependekeza Jenerali Dempsey yafanyike katika kumaliza umwagaji wa damu nchini Syria ni pamoja na kutoa mafunzo, kushauri na kuwasaidia wapinzani, kuanzisha kambi zao ndani ya Syria pamoja na kudhibiti matumizi ya silaha za kemikali. Jenerali Dempsey amesisitiza kitu muhimu kwa sasa kufanyika ni kuimarisha kikosi cha upinzani kinachopigana na Serikali ya Rais Assad ili kuwe na uwezo wa kupambana ikiwa ni pamoja na kupatiwa zana zaidi.
Haya yanakuja kipindi hiki Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa UN Leila Zerrougui akitoa onyo huenda Viongozi wa Serikali na hata wale wanaopingana na Serikali wakakabiliwa na makosa ya uhalifu wa kivita dhidi ya watoto. Mjumbe huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Watoto ameweka wazi pande zote nchini Syria zimeonekana kufanya uhalifu dhidi ya watoto ikiwemo ni pamoja na kusababisha vifo vya watoto. Mapigano hayo yaliyodumu kwa kipindi cha miezi ishirini na nane yamechangia vifo vya watu zaidi ya laki moja huku wakimbizi wanaokaribia milioni moja na laki nane wakipatiwa hifadhi katika nchi jirani za Jordan na Uturuki.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO