Friday, July 05, 2013

JESHI LA MISRI LAWAONYA WAANDAMANAJI WANAOMUUNGA MKONO MURSI

Jeshi la nchini Misri limewaonya wale walio na njama za kufanya mashambulizi ya kulipa kisasi baada ya Jeshi hilo kumuangusha Rais Mohamed Morsi. Jeshi limesema kuwa linaunga mkono haki ya kufanyika kwa Maandamano ya amani lakini limeonya kuwa vitendo vya Ghasia na kutotii sheria kama vile kufunga barabara vitahatarisha amani. Kauli hiyo imekuja baada ya wanamgambo wanaomuunga mkono Morsi katika eneo la Peninsula kutishia kulipa kisasi kutokana na kupinduliwa kwa Rais.
Chama cha Muslim Brotherhood kimeitisha Maandamano kupinga mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa dhidi ya Kiongozi wa Chama chao, na kuwataka Raia kushiriki hii leo baada ya Swala ya Ijumaa. Jeshi limeapa kuwashugulikia watu watakaoandamana na kuleta vurugu na kuongeza kuwa maandamano hayo yanapaswa kuwa ya amani na si vinginevyo. Jeshi la Misri limechapisha taarifa yake kwenye ukurasa wa Facebook likieleza kuwa watu wengi walijeruhiwa katika makabiliano baina ya wafuasi wa Morsi na upande uliokua ukimpinga huko Nile Delta kabla ya kufanyika kwa maandamano ya leo.
Jeshi pia limesema katika eneo la Sinai mwanajeshi mmoja wa Serikali ameuawa mapema leo baada ya watu waliokuwa na silaha kuwashambulia wanajeshi na polisi kwenye uwanja wa ndege.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO